January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wachimbaji wadogo walia na wawekezaji wakubwa

Na Esther  Macha,Timesmajira, Online,Chunya
WACHIMBAJI wadogo katika`wilaya ya Chunya  mkoani  Mbeya  wamelalamikia watu wenye uchumi mkubwa wa kifedha  kuchukua maeneo makubwa  kwa ajili ya  uchimbaji wa madini badala yake maeneo hayo yamekuwa yakikaa bila kufanya  shughuli yeyote ya uzalishaji  hali inayowafanya wachimbaji wadogo kushindwa kuingia katika maeneo hayo kwa ajili ya kutafuta riziki.

Kufuatia hali hiyo kumekuwa na migogoro ya kutishiana ,kuumizana na hata kutoleana lugha za matusi baina ya wachimbaji  kutokana na  wawekezaji  wakubwa  kuchukua maeneo makubwa pasipo kuyafanyia kazi .

Hayo yamesemwa jana mchimbaji mdogo katika kata ya Sangambi , Yususu Mwasenga wakati walipotembelewa na waandishi wa habari wa mkoa wa Mbeya kwa lengo la kujua changamoto za wachimbaji wadogo katika maeneo mbali mbali ya  wilaya  hiyo .

Mwasenga amesema  serikali ilisema  kuwa mwananchi yeyote akipita maeneo ambayo hajapimwa  anaweza kupima kupitia simu yake  ya mkononi akaomba msaada na kupewa eneo hususani maeneo yenye madini ,suala hili limekuwa changamoto  kwa wananchi  kupimwa kwa siri pasipo kuwepo mwenye eneo  hivyo kuwepo mizozo kati ya wananchi na wachimbaji .

“Serikali inasema ukipata eneo kabla kuchukua kibali ongea na mwananchi mwenye shamba  na mkimaliza ndipo unaweza kuchukua kibali cha uchimbaji , lakini kuna watu hawafuati yote haya na hivyo kuwepo kwa mizozo ya mara kwa mara kwenye maeneo ya shughuli za uchimbaji  “amesema Mchimbaji huyo mdogo.

Hata hivyo amesema kitu kingine ni kwa watu wenye uwezo wa kifedha kuchukua maeneo makubwa kwa lengo la kuwekeza kuchimba lakini hachimbi na badala yake anakuwa hafanyi kazi  hivyo kusababisha wachimbaji wadogo kukimbia kukimbia kama swala kutokana na kutokuwa na maeneo ya uchimbaji .

Aidha Mwasenga  ameomba serikali kutoa fursa kwa maeneo yasiyofanya kazi kwa wachimbaji wadogo  ili waweze kuwekeza kwenye vikundi na vyama ,lakini pia serikali iangalie ni wapi itatoa maeneo ya wachimbaji wadogo.

Malongo Asote ni mchimbaji mdogo kata ya Sangambi  ameomba serikali ilegeze masharti ya matumizi ya  baruti  kutokana na kuwa  magumu kwasababu uchimbaji wao lazima watumie baruti  ,tunaelekezwa kujenga maghala ya baruti ambayo ghalama yake ni kubwa ambayo kwa mchimbaji mdogo ni ngumu kumudu ujenzi huo wa maghala.

Aidha Mchimbaji huyo ameomba serikali iwasikilize hasa ukizingatia pato kubwa  la Taifa ni dhahabu ndicho kitu chenye thamani ,kumekuwa na ahadi  nyingi za kumaliza changamoto za wachimbaji wadogo  lakini kumekuwa hakuna utekelezaji  ukija kwenye kodi  nazo zimekuwa nyingi  kwa wachimbaji .

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Chunya ,Tamimu Kambona amesema  kuwa hali ya makusanyo sekta ya dhahabu inakwenda mil.90  kwa mwezi  mpaka mil.100 kwa mwezi.

Kambona amesema kuwa ipo changamoto kubwa kwa wachimbaji wadogo ,wameamua kutafuta maeneo ya uchimbaji na kukabidhi kwa wachimbaji wadogo  watapewa kipaumbele cha kupewa maeneo  ili kuepuka migogoro iliyopo kwa wachimbaji wadogo hasa ukizingatia ndo waliotawala maeneo yote.

“Kikao cha kamati ya ushauri cha wilaya kitakaa na  kuona maeneo ya wachimbaji wadogo  yanatafutwa na kupimwa  hasa ukizingatia asimilia 30 ya mapato ya halmaushauri yanategemea dhahabu “amesema Kambona.
Mwisho.