Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online Tanga
Jumla ya Maafisa Maendeo ya Jamii 12 wamepelekwa kwenye Kijiji cha Msomera mkoani Tanga kwa lengo la kuchechemua shughuli za Maendeleo katika Kijiji hicho.
Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Zainab Chaula ameyasema hayo leo Januari 31, 2023 wakati wa ziara ya siku tatu mkoani Tanga kwaajili ya kuangalia fursa zilizopo kwenye Kijiji hicho.
Dkt. Chaula akiwa na ujumbe wake ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Omary Mgumba amemueleza kuwa ziara hiyo ni sehemu ya Mpango kazi wa Wizara katika kukihudumia Kijiji hicho.
“Mara baada ya Kijiji cha Msomera kuanza kila Wizara ilikuwa na jukumu lake, sisi Wizara yetu tulikabidhiwa jukumu la Maendeleo na Ustawi wa Jamii hivyo tutalitekeleza jukumu hilo kikamilifu” amesema Dkt. Chaula.
Dkt. Chaula ameongeza hadi sasa tayari Wizara imepeleka Maafisa Maendeleo ya Jamii 12 ambao jukumu lao kubwa ni kuchechemua shughuli za Maendeleo kwa kuibua fursa na kuwafundisha ujasiriamali wananchi kijijini hapo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Omary Mgumba, ameishukuru Wizara kwa hatua hiyo na kumhakikishia Katibu Mkuu Dkt. Chaula na ujumbe wake ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yao katika Kijiji hicho.
“Tunaishukuru Serikali kwa kuleta maendeleo ya kasi kijiji cha Msomera, Handeni na hadi sasa huduma zote za kijamii muhimu zinapatikana kijijini hapo.” amesema Mhe. Mgumba
Katika Siku ya kwanza ya ziara hiyo Katibu Mkuu Dkt. Chaula na ujumbe wake wamekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni na Timu ya Menejimenti Wilaya kilipo Kijiji cha Msomera.
More Stories
TASHICO,yatoa ufafanuzi Mv.Serengeti kutitia upande mmoja
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua