January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wachangishana fedha kutengeneza madawati

Na Suleiman Abeid,Timesmajira Online. Shinyanga

WAKAZI wa Kata ya Solwa wilayani Shinyanga, wakishirikiana na Diwani, Awadhi Aboud wamefanikiwa kuchangishana zaidi ya sh. milioni 28.5 na kuweza kutengeneza madawati 336, yaliyomaliza changamoto ya uhaba wa madawati katika Shule ya Sekondari ya Kata na nyingine zitatumika katika ujenzi wa vyoo.

Baada ya kukamilika kwa madawati hayo wananchi hao wamemkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko ambapo kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Solwa, Thomas Manembe amesema kwa sasa shule yake haikabiliwi tena na changamoto ya ukosefu wa madawati na badala yake ina ziada ya madawati 61.

Akipokea madawati hayo Mkuu wa Wilaya, Jasinta amewapongeza wakazi wa kata hiyo kwa jinsi walivyoonesha moyo wa kushirikiana na serikali katika kuhakikisha wanamaliza changamoto ya ukosefu wa madawati kwenye shule yao.

“Nakupongezeni kwa juhudi hizi ambazo mmezionesha kwa sasa, Solwa pamoja na wingi wa wanafunzi wapatao 738, hakuna hata mwanafunzi mmoja anayesoma akiwa amekaa chini, nikupongezeni sana Diwani na Wenyeviti wako wa vijiji, sungusungu na watendaji wengine kwa kusimamia vizuri ukusanyaji wa fedha na kwa uaminifu mkubwa, nawapongeza,” amesema.

Kwa upande wa wanafunzi, Mkuu huyo wa Wilaya amewataka wazingatie suala la elimu na wajiepushe na vishawishi vyovyote, ambavyo vinaweza kuwa chanzo cha wao kufanya vibaya katika masomo yao huku akiwasisitiza zaidi watoto wa kike, ambao mara nyingi hurubuniwa kwa vitu vidogo vidogo na kujikuta wakiacha masomo.

“Watoto wangu ninyi someni kwa bidii, muombeni Mwenyezi Mungu lazima mtafaulu, hakuna anayefaulu bila ya kusoma, achaneni na mambo ya miziki haya mambo ya kamata chini kamata chini sijui nini, hii hapana, waachieni akina Diamond huko, ninyi someni, sisi mnaotuona hapa tulisoma na kuwasikiliza vizuri walimu wetu.

“Jambo lingine ninalosisitiza kwa watoto wa kike someni, msidanganyike na wapita njia wanawapotezeeni maisha yenu bure na Wakuu wa Shule niliishawaagiza muwe mnakaa na hawa watoto wa kike na kuzungumza nao wasikubali kurubunika, watapewa ujauzito na kukimbiwa, watakaohangaika ni wazazi, acheni kudanganywa kwa sh. 2,000 ama simu, someni mtatafuta vya kwenu,” amesema.

Naye Diwani Aboud, amesema mafanikio yaliyowawezesha wananchi kuchanga fedha na kutengeneza madawati 336 na viti vyake yaliyogharimu sh. 23,600,000, yametokana na uongozi mzuri wa Kamati ya Maendeleo ya Kata (WDC) ya Solwa ambapo wananchi walikubali kuuza mali zao ili kupata fedha hizo.

Kwa upande wa suala la afya, diwani huyo amesema wananchi wa Kata ya Solwa wamefanikisha ujenzi wa shule mbili za msingi kwa nguvu zao na kuweza kujenga zahanati mbili katika Vijiji vya Mwakatola na Mwandutu, ambazo tayari zimepauliwa na pia wamekamilisha ujenzi wa chumba kimoja cha maabara katika shule yao ya sekondari.

Awali katika taarifa yake kwa Mkuu wa Wilaya, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Solwa, Thomas Manembe amesema hivi sasa shule hiyo haina tena upungufu wa madawati, baada ya kukabidhiwa madawati yaliyotengenezwa kwa nguvu za wananchi na hivi sasa, wana ziadi ya madawati 61 ambayo yamehifadhiwa kwa matumizi ya baadaye.