January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Katibu Mkuu wizara ya Elimu ,Sayansi na Teknolojia Dkt.Leonard Akwilapo akizungumza na waandishi wa habari(hawapo pichani)

Wabunifu wahamasishwa kushiriki mashindano ya MAKISATU

Na Joyce Kasiki,timesmajira online,Dodoma

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia Dkt.Leonard Akwilapo  amewataka wabunifu kujisajili kwa ajili ya kushiriki kwenye mashindano ya Kitaifa ya Sayansi ,Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU) yanayotarajia kufanyika Machi 20-26 mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma,Dkt.Akwilapo ametoa wito kwa wabunifu kutoka maeneo mbalimbali nchini wajitokeze kwa wingi katika mashindano hayo  huku akisema zoezi la usajili limeanza tangu mwezi Novemba mwaka jana na litaendelea hadi February 15 mwaka huu.

Amesema lengo la mashindano hayo ni kutambua na kuendeleza jitihada zinazofanywa na wabunifu na wagunduzi wa teknolojia nchini ili bunifu hizo zitumike katika kutatua kero mbalimbali katika Jamii.

Katibu Mkuu huyo ametaja washiriki wa mashindano hayo kuwa ni pamoja na makundi ya shule za msingi,sekondari,vyuo vya ufundi stadi,vyuo vya ufundi wa kati,vyuo vikuu,taasisi za utafiti na Maendeleo na Mfumo usio rasmi huku akisema kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘Sayansi ,Teknolojia na Ubunifu kwa uchumi endelevu.

 Dkt.Akwilapo alitumia fursa hiyo kutaja mafanikio yaliyopatikana mwaka 2019/2020 ambapo amesema jumla ya wabunifu wachanga 1066 kati yao wabunifu 130 wameendelezwa na Serikali ili bidhaa zao ziweze kuwa kibiashara na kuwakomboa kiuchumi.

“Bunifu 20 katika ya 130 zinazoendelezwa na Serikali zimefikia hatua ya kubiasharishwa na hivyo kutatua changamoto mbalimbali katika Jamii” amesema Dkt.Akwilapo

Aidha amesema Wizara hiyo imeendelea kuhamasisha wadau wa mashindano hayo ikiwa ni pamoja na kuimarisha uratibu lengo ni kuendeleza bunifu hizo ambazo zinaweza kuibua uchumi endelevu kutoka na Teknolojia inayozalishwa nchini ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo wabunifu.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi (COSTECH)Dkt.Amos Nungu amesema wamekuwa wakiendeleza wabunifu kwa kuwajengea uelewa pamoja na kuwapa mafunzo ili watoke katika ubunifu na wafanye kazi.

Mashindano hayo ambayo yameanza mwaka 2019,ni moja ya mikakati ya Serikali ya awamu ya tano katika kuibua,kutambua na kuendeleza bunifu na ugunduzi unaofanywa na watanzania hususani  wale wa ngazi za chini.