Na Hadija Bagasha, TimesMajira Online
Ili kupunguza mimba za utotoni wananchi wa Kata ya Tongwe wilaya ya Muheza wamejitokeza kufanya msaragambo wa ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa kwa ajili ya kusogeza huduma hiyo karibu na kata yao ambapo hivi sasa wanafunzi wanatembea kwa umbali wa kilomita zaidi ya 19 kufuata elimu kata ya jirani.
Wakizungumza wakati wa zoezi hilo la msaragambo wananchi wa kata hiyo wamesema, lengo lao ni kuhakikisha hadi ifikapo mwakani shule hiyo inaanza na hivyo watakuwa wamemaliza tatizo la wananchi kutembea umbali mrefu.
Wananchi hao wamesema, hivi sasa wanafunzi wao wanapata adha kubwa ya kutembea zaidi ya kilomita 10 kwa ajili ya kufuata elimu katika kata ya jirani, hivyo uwepo wa shule hiyo utaisaidia kupunguza adha hiyo.
“Kutokana na umbali mrefu ambao wamekuwa wakitembea watoto wetu huwa wanapata changamoto njiani kwa kuwa watoto wa kike walikuwa wanapata vishawishi na wakati mwingine wanajikita wakijiingiza kwenye mahusiano wakati wakiwa na umri mdogo, “amesema mmoja wa wazazi.
Kwa upande wake diwani wa kata hiyo ambaye pia ni mwenyekiti wa Halmashauri ya Muheza, Erasto Mhina amesema, wanafunzi wanalazimika kutembea umbali wa kilomita 19 kwa ajili ya kwenda kufuata elimu katika shule iliyopo kata ya jirani jambo ambalo limekuwa pia likisababisha uwepo wa utoro.
Amesema kuwa, pia wanafunzi wamekuwa wakipata matokeo mabaya kutokana na umbali huo, lakini hivi sasa utakapokamilika ujenzi wa shule hiyo utasaidia kuinua ari ya wanafunzi kusoma bila vikwazo.
“Kupitia nafasi yangu niliyo nayo kutokana na changamoto iliyopo niliamua kufanya huu msaragambo ili kuhamasisha wananchi kujenga shule hii kwa haraka na watoto waweze kupata elimu katika eneo la karibi,”amesistiza diwani huyo.
Amesema, shule hiyo itatoa fursa kwa wanafunzi wengi huku kwa kuwa kwa asilimia kubwa watakuwa wamewasaidia wanafunzi wa kike kuondokana na vishawishi huku wakitarajia wanafunzi kufanya vizuri zaidi katika masomo yao na hatimaye kiwango cha ufaulu kupanda.
Kwa upande wake Diwani wa Viti Maalumu kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Ashura Kachenje amesema kuwa, ameamua kushiriki msaragambo huo wa ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa kuwa maendeleo hayana chama.
“Nimekuja kushirikiana na diwani mwenzangu kwa kuwa najua shule hii ikikamilika siyo watoto tu wa CCM watakuja kusoma bali watakuja ma wa vyama vyote vya upinzani natoa wito kwa wananchi wenzangu na viongozi kujitoa kwa wingi kwenye kazi za maendeleo kwa kuwa maendeleo hayajalishi chama gani, “amesema.
More Stories
Jokate awapa tano vijana UVCCM maandalizi Mkutano Mkuu wa CCM
Watakaokwamisha mapato Kaliua kukiona cha moto
Dkt.Gwajima aagiza kuundwa kamati za ulinzi wa watoto