December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waanza kutoa mafunzo uhifadhi, usindikaji nyanya

Na Mwandishi Wetu,Timesmajira Online. Morogoro

SHIRIKA la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) Mkoa wa Morogoro, limewawezesha kupata jokofu la asili la kutunzia nyanya na mazao ya mboga mboga, sambamba na kuwapatia mafunzo ya usindikaji wa zao la nyanya wakulima wa Kata ya Dumila Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro.

Akizungumza na wakulima hao Dumila jana Meneja wa SIDO Mkoa wa Morogoro, Haika Shayo amesema shirika hilo pamoja na majukumu mengine yenye lengo la kuendeleza viwanda vidogo, lina wajibu pia wa kutoa huduma ya tenkolojia na ufundi kwa ajili ya kuongeza thamani bidhaa na malighafi mbalimbali zinazozalishwa na wananchi, ili ziweze kukidhi vigezo na kuyafikia masoko yenye tija.

“Katika kutekeleza dhana hiyo, tumewawezesha wakulima wa Dumila ambao wanajishughulisha na kilimo cha nyanya na mboga mboga kuweza kuwa na jokofu asilia kwa ajili ya kuhifadhi nyanya kwa muda mrefu, ili zisiweze kuharibika na kuweza kuyafikia masoko yenye tija,” amesema.

Shayo ameongeza kuwa sambamba na hayo, SIDO imewapatia mafunzo wakulima hao ya kusindika nyanya na kutengeneza bidhaa mbalimbali zinazotokana na zao hilo kama vile, sharobati ya nyanya, waini ya nyanya, jam, tomato sosi na bidhaa nyingine.

Kwa upande wake, Joan Nangawe Ofisa Uendelezaji wa Tenkolojia ya Chakula SIDO Mkoa wa Morogoro amesema shirika hilo, linashiriki programu ya uendelezaji na ukuzaji wa ujuzi waliandika andiko lililowawezesha kuandaa utengenezaji wa majokofu ya asili katika kupunguza upotevu wa mali mbichi kwa sababu ya kukosa teknolojia za uhifadhi na usindikaji wa mazao hayo.

Nangawe amesema eneo la Dumila ni eneo ambalo linazalisha nyanya na mboga mboga kwa wingi, ambapo wakulima walikuwa wakikabiliwa na upotevu mkubwa wa mazao hayo kwa kuwa yalikuwa yakiharibika kabla ya kufikishwa sokoni kwa kukosa eneo maalumu la kuhifadhia ili yadumu kwa muda mrefu.

“Jokofu hili lina uwezo wa kuhifadhi nyanya tani moja sambamba na mboga mboga nyingine na zinaweza kukaa humu kwa muda wa siku 14 pasipo kuharibika, hivyo unaweza kuona ni kiasi gani wakulima hawa wanaweza kuokoa uharibifu wa mazao yao wakati wanasubiri kusindika au kupeleka sokoni,” amesema.

Joan amesema jokofu hilo, linatumia teknolojia ya kiasili kwa kutumia malighafi za gharama nafuu na ana uhakika kuwa, wakulima wa Dumila na maeneo mengine mkoani Morogoro watapata mwamko wa kujifunza na kuitumia teknolojia hiyo, ili waweze kuhifadhi mazao yao ya mboga mboga kwa muda mrefu.

Naye Mwenyekiti wa kikundi cha wazalishaji wa zao la nyanya na mboga mboga Dumila, Mpondomoka Ramadhani amesema SIDO imewasidia kurudisha matumaini yao ya kuzalisha kwa tija na kupata masoko ya uhakika, hivyo watakuza vipato vyao na kuboresha hali zao za maisha.

“Kipindi cha msimu wa mavuno ya nyanya hapa kwetu Dumila, tulikuwa tunapata hasara kubwa kwa kuwa nyanya nyingi huozea shambani kwani huwezi kuvuna kama huna soko na ikiwa utavuna, hakuna pa kuzihifadhi ili zisiharibike pia hatukuwa na ujuzi wa usindikaji,” amesema.

Ameongeza kuwa wanaishukuru SIDO kwa kuwapatia elimu ya kusindika zao la nyanya na kuwasaidia kupata jokofu, ambalo kwao ni mkombozi mkubwa kwa kuwa wana uhakika sasa mazao yao hayataharibika tena.