November 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waangalizi Uchaguzi wapongeza vyombo vya habari

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online.

WAANGALIZI wa Uchaguzi Centre for International Policy Africa (CIP), imevipongeza vyombo vya habari kwa ushiriki wake kwenye Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 28, ikilinganishwa na mwaka 2015.

Kauli hiyo ilitolewa juzi jijini Dar es Salaam na Rais na Ofisa Mtendaji Mkuu wa CIP, Omar Mjenga ambaye amesema kazi kubwa ilifanywa na vyombo vya habari ikilinganishwa na 2015.

Amesema ilikuwa ni ruksa kwa mikutano ya vyama mbalimbali vya siasa, mikutano yao kurushwa moja kwa moja kwenye vyombo mbalimbali vya habari ikiwemao Televisheni ya Taifa TBC.

“Tunavipongeza vyombo vya habari kwa kazi kubwa ambayo vilifanya katika kuhakikisha kuwa vinaupasha umma wa Watanzania, juu ya mikutano mbalimbali ya kampeni kwa vyama vyote.

“Hili ni jambo la kupongezwa licha ya kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa baadhi ya vyama vya siasa kuhusu kutokurushwa kwa mikutano yao, lakini kulikuwa na mwamko chanya,” amesema.

Amesema pamoja na kukamilika kwa uchagzi huo, lakini bado kulikuwa na changamoto kwa baadhi ya wasimamizi kutokuwa na elimu ya kutosha juu ya Uchaguzi huo Mkuu.

“Kuna mambo mengi ambayo yameweza kujitokeza ikiwa ni pamoja na kutokuwa na elimu ya kutosha kwa baadhi ya wasimamizi wa uchaguzi, hali iliyoleta changamoto.

“Hivyo tuitake Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na ile ya Zanzibar (ZEC) kufanyia kazi eneo hilo ili kuondoa mkanganyiko,” amesema Mjenga.

Amesema kulikuwa na changamoto ya ukosefu wa elimu ya kutosha kwa wapiga kura kuhusu uchaguzi, jambo ambalo lililosababisha wengi kushindwa kutimiza haki yao ya kikatiba.

“Tunashauri NEC na ZEC kusimarisha utoaji wa elimu ya upigaji kura kwa wananchi katika chaguzi zijazo, hii itasaidia kuimarisha uelewa wao kuhusu uchaguzi, pia kwa baadhi ya wasimamizi wa uchaguzi walionekana kutokuwa na uelewa kuhusu wasimamizi wa uchaguzi, hatua mbayo ilisababisha baadhi kushindwa kuingia kwenye maeneo ya kupigia kura licha ya kuwa na barua kutoka NEC,” amesema.

Katika uchaguzi huo, Rais Dkt. John Magufuli alifanikiwa kutetea nafasi hiyo akimuacha mpinzani wake wa karibu, Tundu Lissu.