Na Penina Malundo, Timesmajira
WAANDISHI wa habari wa mkoa wa Dar es Salaam wameshauriwa kuendelea kuandika habari zinazowahusu Wanawake na Vijana ili kuamsha hamasa ya kuingia katika nafasi za uongozi bila kuangalia changamoto zozote zinazowakabili ikiwemo ukosefu wa fedha.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Kinondoni,Alex Ntiboneka katika mafunzo ya siku moja ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam,alisema uandikaji wa habari za wanawake na vijana kwa wingi utaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa makundi hayo kuingia katika nafasi za uongozi bila kuwa na hofu wala woga wowote.
Amesema tayari shirika la Mazingira na Haki za Binadamu (Envirocare) ni miongoni mwa shirika lililofanya utafiti kujua kwanini vijana na wanawake wengi hawapo katika nafasi ya uongozi na kutokana na vijana wengi kuonekana kutokuwa na busara huku wanawake kuonekana kutoaminika.
”Warsha hii ni nzuri kwa vyombo vya habari katika kuandika na kuripoti masuala ya nafasi za uongozi kwa wanawake na vijana kwani ukiangalia wanawake wamekuwa wakihofia kugombea nafasi le Kinondoni katika kata 20 tuna mwanamke mmoja tu ndo aliyegombea na kuchaguliwa ila kwa madiwani wengine wote ni vitimaalum,”amesema na kuongeza
”Ile dhana ya kusema masuala ya uongozi ni lazima uwe na kipato katika kugombea,waondokane nayo kwani Serikali imeweka mazingira mazuri ya mifumo ya kuwawezesha Vijana na Wanawake lakini baadhi ya watu wanaotoka katika makundi hayo kutotumia ipasavyo,”amesema.
Ntiboneka amesema vikwazo hivyo vya kifedha katika masuala ya uongozi yasiwe vyanzo vya wao kurudi nyuma na kukata tamaa katika kugombea nafasi hizo.”Waandishi sasa ni wakati wa kubadilisha jamii zetu kwa kuandika habari za kinamama vizuri kuhusu masuala ya uongozi na endapo anakosea asihusishe na jinsia yake,”amesema.
Amesema ni wakati sasa wa kupata viongozi wengi wanawake na vijana kwa nafasi za kugombea na zisiwe zile za upendeleo kwao ili kuonyesha jamii nao wanaweza katika kupambania nafasi hizo.
Kwa Upande wake Mratibu wa Shirika hilo la Envirocare ,Godlisten Muro amesema shirika lao linafanya mradi wa kuhamasisha ushiriki wa wanawake na vijana kwenye nafasi za uongozi mkoa wa Dar es Salaam uliochini ya ufadhili wa shirika la Eastern and Central Africa (Forum CIV) ambapo lengo la mradi huo kukuza usawa wa kijinsia na kuongeza ushiriki wa wanawake na vijana katika mfumo wa uongozi kwa mkoa wa Dar es Salaam.
“Mradi huu tunaofanya mkoani Dar es Salaam katika Wilaya ya Kinondoni na Ubungo lengo likiwa ni kuongeza ushiriki wa wanawake na vijana katika mchakato wa maamuzi ifikapo mwaka 2024 hususani katika chaguzi za Serikali za Mitaa,”amesema na kuongeza
”Mradi huu ulianza kutekelezwa kuanzia Aprili 2023 na unatarajia kumalizika Septemba 2024 ambapo katika maswali ya awali waliyoulizwa vijana kwanini ushiriki wao mdogo katika masuala ya uongozi, wengi wao walisema wanaonekana wengi wao hawana busara kabisa huku wanawake wengi walionekana kutoaminiwa,”amesema Muro.
Aidha amesema matarajio yao makubwa ni kuona uelewa unaongezeka katika ushiriki wa uongozi kwa wanawake na vijana kuongezeka na kuona hali ya kuchagua na kuchaguliwa ni haki yao.”Tunamatarajio makubwa na huu mradi tunataka kuona ushiriki wa vijana na wanawake katika vyombo vya maamuzi unaongezeka na uwajibikaji pamoja na mfumo wa utawala unaimarishwa ipasavyo,”amesema.
Muro amesema takribani wanufaikaji wa mradi huo 500 wameweza kushiriki mradi huo huku wanawake wakiwa 300 na vijana 200.
More Stories
Wakuu wa Wilaya,Wakurugenzi watakiwa kusimamia programu za chakula shuleni
Mbowe akuna wengi kuhusu maridhiano
Waziri Chana amuapisha Kamishna uhifadhi NCAA, ampa maagizo mazito