November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waajiri nchini watakiwa kusimamia sheria, kanuni na miongozo

Na Mwandishi wetu, Timesmajira online

WAAJIRI nchini wametakiwa kuzingatia Sheria, Kanuni, na Miongozo inayoongoza Ulimwengu wa Kazi ili kuhakikisha haki, heshima na maslahi ya Wafanyakazi nchini vinastawi na kuondoa migogoro na mifarakano isiyo na tija.

Hayo yamebainishwa Jijini Dar es salaam katika Mkutano wa Chama cha wafanyakazi wa Viwanda, Biashara,Taasisi za kifedha, Huduma na Ushauri TUICO na Waandishi wa Habari uliofanyika kufuatia habari iliyochapishwa kwenye mitandao ya kijamii Machi 23, 2022 iliyowekwa na Said Ibrahim Stawi aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa TUICO kiwanda cha SBC Tanzania Limited Dar es Salaam, aliyeibua suala la Ukiukwaji wa Sheria za Kazi katika kiwanda hicho.

Akizungumza katika Mkutano huo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa TUICO, Wakili Noel Nchimbi ambaye ni Mkuu wa Idara ya Sheria amesema Machi 28 mwaka huu Ofisi ya Katibu Mkuu TUICO, Katibu wa TUICO Kanda ya Dar es Salaam, Uongozi wa SBC Tanzania Limited na Ofisi ya Kamishina wa Kazi Nchini walikaa Kikao cha Ndani kutafuta muafaka wa pamoja kuhusu changamoto zilizoibuliwa.

Amesema baada ya kikao hicho kuna hatua ambazo zimeshaanza kuchukuliwa; na TUICO na kuhaidi kuendelea tutaendelea kutoa ushirikiano ili kutekelekeza makubaliano hayo ili haki, heshima, na maslahi vizidi kustawi na Wafanyakazi watambue wajibu, sambamba na kuheshimiwa kwa Mkataba wa Hali Bora za Kazi uliofungwa kati ya TUICO na SBC Tanzania Limited.

“Chama cha Wafanyakazi TUICO kilibaini kuwa tuhuma zilizoibuliwa na Ndugu Said Ibrahim Sitawi aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa TUICO katika Kiwanda hicho, siyo kauli ya TUICO bali ulikuwa utashi wa aliyezungumza”amesema Wakili Nchimbi

Amesema Kwa mujibu wa Katiba ya TUICO, Msemaji wa Chama ni Katibu Mkuu, na Chama bado kina mahusiano mazuri na SBC Tanzania Limited.

Alibainisha kuwa Chama cha TUICO kimeendelea na utoaji wa elimu kwa Wafanyakazi kuhusu Viwango vya Ajira hali ambayo imeongeza uelewa wa masuala mbalimbali ya ajira sambamba na utendaji mzuri wa kazi hali inayofanya TUICO kuwa na Mikataba hai ya Hali Bora za Kazi zaidi ya 150 katika maeneo mbalimbali ya kazi ambayo ni matokeo ya ushirikiano mzuri katika yake, Waajiri, na Serikali.

Aidha, TUICO imelaani vikali vitendo vya unyanyasaji na ukatili wa aina yoyote unaojitokeza kwenye maeneo mbalimbali ya kazi nchini na kusema kitaendelea kutoa elimu kwa Wanachama na Wafanyakazi kuhusu aina mbalimbali za unyanyasaji ikiwa ni pamoja na unyanyasaji wa kijinsia na kingono ikiwa ni pamoja na kujenga mifumo rafiki ya kuripoti visa hivyo.

Katika Mkutano huo umehudhuriwa na Ofisi ya Kamishina wa Kazi nchini, Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO), Mwakilishi wa SBC Tanzania Limited, sambamba na Wanahabari kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini.

Wakili Noel Nchimbi ambaye ni mkuu wa idala ya sheria TUICO akizungumza na waandishi wa habari