November 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waadhimisha muungano kwa kuchimba msingi wa jengo la mama na mtoto

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

MKUU wa Wilaya ya Magu, Salum Kalli amewaongoza wananchi wa Kijiji na Kata ya Shishani kuadhimisha miaka 58 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa kujitolea kuchimba msingi wa jengo la Mama na Mtoto la kituo cha afya.

Pia wananchi hao wamempongeza na kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan,kwa kuwaletea fedha sh.milioni 250 za tozo ya miamala ya simu kutekeleza mradi huo utakaohudumia wagonjwa 33,822 kutoka wagonjwa 6,588 wa sasa.

Akizungumza juzi kwa niaba ya wananchi hao,Diwani wa Kata ya Shishani (CCM) John Ngagaja,alisema wanamshukuru Rais Samia kutoa fedha kutekeleza mradi huo utakaoboresha huduma za afya ya mama na mtoto wakiwemo wananchi wa vijiji vya kata hiyo.

“Mkusanyiko wa wananchi walijitokeza kuchimba msingi wa mradi huu ni ishara ya kuupokea,kumshukuru na kumpongeza Rais Samia kwa kuwaletea fedha na kuwasogezea huduma karibu, tutatibiwa hapa hapa sisi,wake na watoto wetu,”alisema.

Gangaja aliishukuru serikali kuwaletea mamilioni ya fedha kujenga jengo la wagonjwa wa nje (OPD),upasuaji (Theatre)na kichomea taka na kuomba iwasaidie kuezeka maboma yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi wa kata hiyo.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Shishani,Sara William pamoja na Musa Maganga(73) walisema mradi huo umewaondoa kwenye changamoto ya nauli na kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za mama na mtoto,utakapokamilika utakuwa mkombozi wao na utawawezesha kupata huduma karibu.

Kwa upande wake,Kalli alisema wananchi kuadhimisha miaka 58 ya muungano kwa kuchimba msingi wa mradi wa mama na mtoto na kuacha usingizi,wanaiunga mkono serikali ya awamu ya sita kwa vitendo kwa inayoyafanya kwa maendeleo yao.

“Niwashukuru kujitokeza kwenu kwa wingi kuja kushiriki mwanzoni mwa mradi huu,endeleeni na moyo huo, tushirikiane kwa uzalendo huo,umoja na utaifa wetu, CCM ilitupatia ilani kuhakikisha sekta ya afya inaboreshwa wananchi wanakuwa afya bora ndicho serikali kwa pamoja tunachokifanya hapa leo,”alisema mkuu huyo wa wilaya.Alisema afya ni mtaji wa kila mmoja bila afya bora hakuna maendeleo na Mh.Rais Samia amewekeza sh.milioni 500 katika Kijiji na Kata ya Shishani wananchi wahudumiwe karibu kwenye miundombinu bora,hivyo kushiriki kwao kuchimba msingi wameonyesha ishara ya upendo kwa serikali ya awamu ya sita.
Aidha mkuu huyo wa wilaya aliwahimiza wananchi hao kujitokeza kuhesabiwa siku ya Sensa na Makazi ili kumpa Rais Samia nguvu ya kutafuta,pia watoto wa umri chini ya miaka mitano wapelekwe kupata chanjo ya polio na kuwataka waepuke uzushi kuhusu chanjo hiyo.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Magu (DED),Federica Myovella alisema,serikali ilitoa sh.milioni 250 za ujenzi wa OPD, jengo la upasuaji na Insinlator, hivyo uhitaji wa wa majengo ya huduma za afya kwa wananchi wa Shishani awamu ya pili imeongeza sh.milioni 250 za kujenga jengo la mama na mtoto.Alisema fedha hizo zitaimarisha miundombinu ya majengo ili huduma zote za dharura zikiwemo za upasuaji zipatikane kituoni hapo kwa wakati na kuwataka wananchi wajiepushe na matumizi mabaya ya fedha hizo,zisimamiwe zitumike vizuri ambapo nguvu kazi yo itathaminishwa.ssssPICHADSC09441-Mkuu wa Wilaya ya Magu, Salum Kalli (katikati), kulia Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya hiyo (DED) Federica Myovella wakishiriki kuchimba msingi wa mradi wa Jengo la Mama na Mtoto katika kituo cha Afya Shishani jana.  

Wananchi wa Kata ya Shishani wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Magu, Salum Kalli (mwenye kapelo) kuchimb msingi wa Jengo la Mama na Mtoto la Kituo cha Afya Shishani jana wakati wa maadhimisho ya miaka 58 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Magu,ikishiriki kuchimba msingi wa mradi wa Jengo la Mama na Mtoto jana ,wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Salum Kalli (wa pili kutoka kulia), wa kwanza ni Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya hiyo (DED) Federica Myovella
Mkuu wa Wilaya ya Magu (mwenye overoll) akizungumza na wananchi (hawapo pichani)baada ya kukamilisha shughuli ya kuchimba msingi wa mradi wa Jengo la Mama na Mtoto katika Kituo cha Afya Shishani ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 58 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar jana
Wananchi wakisaidiana na Mkuu wa Wilaya ya Magu,Salum Kalli,kuchanganya zege kwa ajili ya ujenzi wa msingi wa Jengo la Mama na Mtoto katika Kata ya Shishani, wakati wa maadhimisho ya miaka 58 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar jana
Mmoja wa wananchi wa Shishani na Mkuu wa Wilaya ya Magu,Salum Kalli, wakiwa wamebeba ndoo ya zege jana wakielekea kumwaga kwenye msingi wa mradi wa ujenzi wa Mama na Mtoto, wakati wa maadhimisho ya miaka 58 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar jana