January 17, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Vyuo vya maendeleo ya jamii kupambana na vitendo vya ukatili

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Vyuo vya Maendeleo ya Jamii vinavyosimamiwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum vimejipanga kuweka mikakati ya kufanya Tafiti mbalimbali katika jamii zitakazosaidia kuondokana na vitendo vya ukatili nchini.

Hayo yamebainika wakati wa Kikao kazi cha Utekelezaji wa shughuli za Taaluma katika Taasisi na Vyuo vya Maendeleo ya Jamii kinachofanyika kwa siku Sita jijini Dodoma.

Akizungumza katika kikao hicho Mkurugenzi Msaidizi Vyuo vya Maendeleo ya Jamii kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Bi. Neema Ndoboka Vyuo hivyo vinatarajiwa kuwa na tafiti zitakazotoa suluhisho la uwepo wa vitendo vya ukatili vinavyotokea katika jamii.

Ameongeza kuwa wataalam wa kada ya Maendeleo ya Jamii ndio chachu ya mabadiliko katika jamii hivyo wakitumika vyema na kuwa na tafiti hizo itasaidia kupata namna bora ya kupambana na vitendo vya ukatili hasa katika kuibadilisha Jamii kupambana ba vitendo hivyo.

“Sisi kama wanataaluma tuna nafasi kubwa ya kusaidiana na jamii kupambana na vitendo vya ukatili kwani tunaweza kuja na tafiti nzuri zitakazosaidia kuondoka na vitendo hivi” alisema Bi. Neema.

Kwa upande wake Mtaalam wa Masuala ya Uongozi kutoka Chuo cha Utumishi wa Umma Jesse Mashimi amesema Vyuo vya Maendeleo ya Jamii nchini vinaweza kuleta mabadiliko katika jamii na uelewa kuhusu madhara ya vitendo vya ukatili wa kijinsia katika maendeleo na ustawi wa Jamii.

Wakuu wa Vyuo vya Maendeleo ya Jamii vinavyosimamiwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalum wanakutana jijini Dodoma kwa siku sita katika Kikao kazi cha Utekelezaji wa shughuli za Taaluma katika Taasisi na Vyuo vya Maendeleo ya Jamii kinacholenga kuweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha Taaluma ya Maendeleo ya Jamii inakuwa chachu ya mabadiliko katika jamii.

Mkurugenzi Msaidizi Vyuo vya Maendeleo ya Jamii kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Bi. Neema Ndoboka akieleze lengo la Kikao kazi cha Utekelezaji wa shughuli za Taaluma katika Taasisi na Vyuo vya Maendeleo ya Jamii kinachofanyika Jijini Dodoma.
Mtaalam wa Masuala ya Uongozi kutoka Chuo cha Utumishi wa Umma Jesse Mashimi akitoa mada ya Uongozi katika Kikao kazi cha Utekelezaji wa shughuli za Taaluma katika Taasisi na Vyuo vya Maendeleo ya Jamii kinachofanyika Jijini Dodoma.
Baadhi ya Wakuu na Manaibu Wakuu wa Vyuo vya Maendeleo ya Jamii vinavyosimamiwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum wakiwa katika Kikao kazi cha Utekelezaji wa shughuli za Taaluma katika Taasisi na Vyuo vya Maendeleo ya Jamii kinachofanyika Jijini Dodoma.