December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Vyuo vikuu nchini vyatakiwa kutenga fedha kugharamia masuala ya utafiti na ubunifu

Na Irene Clemence, TimesMajira Online

VYUO Vikuu vyote nchini vimetakiwa kutenga fedha kutoka katika vyanzo vya mapato ya ndani kwaajili ya kugharamia masuala ya utafiti na ubunifu.

Kauli hiyo ameitoa Jijini Dar es salaam leo na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omari Kipanga wakati akifungua maadhimisho ya saba ya wiki ya utafiti na ubunifu kwa niaba ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Alisema ili kuhakikisha mchango wa utafiti na ubunifu unadhihirika katika kuhakikisha maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa jamii, ni vyema zikalenga katika kutatua changamoto zinazolenga jamii moja kwa moja, kwani zitarahisisha na kusaidia jamii badala ya kubaki kwenye makaratasi.

Hivyo aliagiza wiki ya utafiti na ubunifu iendelee kuadhimishwa kila mwaka na vyuo vikuu vyote nchini.

Alisema kwa kufanya hivyo kutaongeza hamasa ya kufanya utafiti na ubunifu wenye tija nchini na kutoa nafasi kwa wabunifu wachanga na wengi kujitokeza kuonesha bunifu na Teknolojia zao.

“Pia kukutana na watumiaji wa bidhaa zinazotokana na utafiti na ubunifu na hivyo kuongeza fursa za kiuchumi kwa vijana na kukuza vipaji vyao.

“Pia vyuo vikuu vyote nchini vitenge fedha kutoka katika vyanzo vya mapato ya ndani kwaajili ya kugharamia masuala ya utafiti na ubunifu. Imeelezwa kuwa UDSM imeshaanza kutekeleza hilo, na wengine muendelee kufanya hivyo mwaka hadi mwaka,” alisema.

Pia aliagiza vyuo vikuu kupitia vitengo vya utafiti, waelimisheni watafiti na wabunifu kuhusu umuhimu wa kulinda matokeo ya utafiti na ubunifu kwa kupewa haki miliki

“Elimu hiyo ni muhimu kwani itawawezesha watafiti wetu kulinda bunifu zao. Wekeni mikakati ya kuwaelimisha watafiti na wabunifu wachanga kuhusu umuhimu wa mambo haya,” alisema.

Vilevile, aliziagiza Taasisi za utafiti na maendeleo zishirikiane na sekta binafsi hususani viwanda, ziweke utaratibu wa kuendeleza matokeo ya tafiti na bunifu zinazozalishwa nchini na kuhamasisha matumizi yake ili kuongeza kasi ya maendeleo ya jamii na uchumi.

“Hapa tunacholenga sisi ni kuona matokeo ya tafiti na bunifu unaendelezwa, unafatiliwa na kuratibiwa sambamba na kuwasaidia katika bunifu zao,” alisema Kipanga.

Naye Makamu Mkuu wa Chuo UDSM, Profesa William Anangisye alisema katika kutambua umuhimu wa Ubunifu na utafiti katika kutatua chagamoto zinazoikabili jamii ya Tanzania na Taifa kwa ujumla chuo Kikuu Cha Dar es salaam kimekuwa kikitenga bajeti kwa kutegemea vyanzo vya ndani.

Alisema kwa mwaka wa fedha 2018/2019 chuo kikuu cha UDSM kilitenga billioni 1 kwa ajili ya utafiti na Ubunifu.

“Idadi ya fedha za Ubunifu na utafiti zimekuwa zikiongezeka hadi kufikia Billion 1.4 kwa mwaka 2019/20 na shilingi billlioni 1.9 kwa mwaka 2020/21 na Billion 3.1.5 kwa mwaka wa fedha 2021/22″alisema

Alisema fedha zote hizo ziligawiwa kwa wanataaluma na kuwasilisha mapendekezo ya utafiti na miradi mbalimbali .

Aliongeza kuwa mwaka 2015 UDMS ilianzisha wazo la kuwa na wiki ya utafiti ili kukuza na kuonesha matokeo ta tafiti zake kwa jamii ambayo imelenga kuweka bayana tafiti na bunifu mbalimbali.

Naye mtoa mada katika maadhimisho hayo mfanyabiashara Seif Seif alisema suala la ajira limekuwa ni chagamoto kubwa hivyo amewataka wadau kwa ujumla kushirikiana ili kuweka mkakati wa pamoja ambayo ni bora na kuleta tija.

Alisema ajira zimekuwa zipo ila chagamoto kubwa imekuwa kupata watu wenye ujuzi wa kutosha ambao wataweza kukidhi mahitaji.

“Ajira zipo ila tumekuwa hatuna watu wenye ujuzi wa kutosha ambao wanaweza kukidhi maitaji husika” alisema Seif.

Naibu waziri elimu sayansi na Teknolojia Omari kipanga akizungumza katika maadhimisho hayo
Makamu Mkuu wa chuo UDSM Profesa William Anangisye akizungumza katika maadhimisho hayo