Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Moshi
Vyombo vya Watumia Maji vya jamii (CBWSOs) vinavyosimamiwa na Wakala ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), vimetakiwa kutumia Mfumo wa pamoja wa Ankara za Maji (MAJIIS), ili kuongeza ufanisi katika utendaji kazi pamoja na kuimarisha utoaji wa huduma ya maji kwa wananchi.
Agizo hilo limetolewa hivi karibuni na Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Kisare Makori, wakati akifunga mafunzo ya siku saba kwa Maafisa wa CBWSOs wa mkoa wa Kilimanjaro yaliyofanyika katika ukumbi wa Chuo cha USHIRIKA mjini Moshi .
Amesema, Serikali imedhamiria kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika taasisi za umma ili kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi kwa urahisi, haraka na kwa gharama nafuu mahali walipo.
“Serikali ya awamu ya sita inachukua jitihada mbalimbali katika kuhakikisha TEHAMA inarahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi, ambapo kupitia Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kwa kushirikiana na Wizara ya Maji, imetengeneza mfumo wa MAJIIS ili kutatua changamoto mbalimbali zilizokua zinaikabili Sekta ya Maji”, amesema.
Amefafanua kuwa, Serikali imewekeza katika mfumo huo hivyo ni jukumu la watumishi wa sekta ya Maji kufanya kazi ili kuhakikisha mfumo huo unakua mkombozi kwa wananchi.
Kwa upande wake mtaalamu wa TEHAMA kutoka Wizara ya Maji Mha.Masoud Almas amesema, mfumo wa MAJIIS umeboreshwa ili uweze kutumiwa na Vyombo vya Watumia Maji vya jamii (CBWSOs) vinavyotoa huduma vijijini ili kuhakikisha TEHAMA inarahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi mahali walipo.
“Mkoa wa Kilimanjaro umekuwa ni mkoa wa kwanza kuanza kutumia mfumo huu wa MAJIIS kwa CBSWOs na Wizara itaendelea kuhakikisha CBSWOs zote katika mikoa mingine zinatumia mfumo huu ili kurahisisha utendaji kazi na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi waishio vijijini”amesema.
Ameongeza kuwa, hadi sasa mfumo huo umeleta mafanikio makubwa kwa Wizara ya Maji ikiwa ni pamoja na kuongeza ukusanyaji wa mapato na kurahisiha upatikanaji wa taarifa za Mamlaka zote za Maji nchini.
“Hadi sasa, Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingiara za miji mikuu ya mikoa, miradi ya kitaifa, miji ya Wilaya na miji Midogo 87 Tanzania Bara na Zanzibar pamoja na Bodi za Maji za Mabonde 9 zinatumia Mfumo huu wa Pamoja”, amefafanua Almas.
Aidha,amebainisha kuwa ili kuongeza ufanisi katika utendaji kazi, mfumo wa MAJIIS umeunganishwa na mifumo mingine ya Serikali ikiwa ni pamoja na mfumo wa GePG, Mfumo wa Barua Pepe Serikalini (GMS), Mfumo wa Ujumbe Mfupi wa Simu za mkononi ambao hutumika kutoa taarifa za huduma kwa Wateja ikiwemo kutuma bili, mfumo wa NIDA na mfumo wa BRELA.
Jumla ya washiriki 72 kutoka Vyombo vya Watumia Maji vya jamii (CBWSOs) 39 vya mkoa wa Kilimanjaro walihudhuria mafunzo hayo.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato