May 25, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Vyama vya Ushirika Katavi vyatakiwa kuthibiti utoroshaji mazao

Na George Mwigulu,Timesmajiraonline,Katavi

WAKULIMA wa zao la Tumbaku mkoani Katavi wameonywa kuwa sehemu ya utoroshaji wa zao hilo katika Vyama Vya Msingi vya Ushirika ili kuepusha vyama hivyo kuingia hasara na kulimbikiza madeni.

Imetajwa kuwa baadhi ya wakulima mkoani Katavi wasiyo waaminifu wamekuwa na desturi isiyo nzuri ya kuchepusha zao la tumbaku wakati wa mavuno na kuuza mahala kwingine kinyume na sheria,taratibu na miongozo ya Ushirika jambo ambalo moja kwa moja linadhorotesha ukuaji wa sekta ya kilimo cha zao la tumbaku.

Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Jamila Yusuph akizungumza Mei 23, 2025 katika ukumbi wa Mpanda Social Hall wakati wa mkutano wa Jukwaa la nne la Maendeleo ya Ushirika Mkoani Katavi amesema wakulima wa zao la tumbaku wanapaswa kuheshimu miongozo ya Ushirika kwa ajili ya faida yao na taifa.

Kiongozi huyo wa Wilaya akimwakilisha Mkuu wa Mkoa Katavi wakati wa mkutano huo, amebainisha kuwa tatizo la utoroshaji wa tumbaku kwa baadhi ya wakulima huleta athari kwa wakulima waaminifu ambao kuwajibika kulipa madeni kwa taratibu za Ushirika na baadhi yao kushindwa kuendelea na kilimo hicho.

Katika kudhibiti utoroshaji huo amesema bado ipo nafasi ya kuwabaini wanaotorosha kwani uwezo na nguvu zipo kupitia vyombo vya dola ili kusaidia kuondoa tatizo hilo.

Vile vile ameeleza kuna haja ya kufanya uchunguzi kwa wale ambao wanapokea ziada ya uzalishaji wa tumbaku kwani kunauwezekano ziada hiyo inatokana na utoroshaji wa tumbaku kutoka mahala pengine.

“Hawa wanaofurahia kupokea ziada najua kunamanufaa yanakuja baadae kwa kupokea ziada lakini lazima kuchunguza hii ziada wanayoipata inatokea wapi ili tusiwaumize wakulima wetu,”amesema Jamila.

Katika hatua nyingine Jamila amesema dhamira ya serikali inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamuhuri ya Muugano wa Tanzania ya kuipeleka nchi kwenye uchumi wa viwanda ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuongeza kasi ya maendeleo kufikia lengo la dira ya taifa ya maendeleo ya mwaka 2025.

Malengo hayo yanaweza kufikiwa kama Ushirika utakuwa imara kwa kuwepo katika nyanja zote za uchumi na uzalishaji. Na kwa umuhimu huo serikali itaendelea kuboresha mazingira rafiki ya kisera, sheria na kanuni ili vyama vya ushirika mkoani Katavi vifanye kazi kwa ufanisi.

Aidha ametoa maelekezo kwa taasisi zinazohusika na Ushirika ni Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania kuongeza kasi ya usimamizi wa vyama vyote vya ushirika kwa kuhakikisha vinajiendesha kwa mujibu wa sheria.

Tume ya Maendeleo ya Ushirika Mkoa wa Katavi kwa kushirikiana na wadau wengine kuhamasisha zaidi uanzishwaji wa vyama vya akiba na mikopo kutokana na vilivyopo ni vidogo, hali yake hailizishi na uwezo wake wa kujiendesha bado ni mdogo.

Kwa vyama vya Ushirika kuimarisha matumizi na mifumo ya kidigitali ili kuwahudumia wananchama kwa haraka, ufanisi, usahihi na kupunguza manung’uniko miogoni mwao. Pamoja na kuimarisha mifumo ya udhibiti wa shughuli zinazofanywa na watendaji kwa kuanzisha kamati na wakaguzi wa ndani.

“Mnatakiwa kubuni vyanzo mbalimbali vya mapato likiwemo suala la uwekezaji wa malimbikizo ya faida zenu kwenye taasisi zinazotoa gawio zuri kwa wawekezaji wake” Amesema Mkuu wa wilaya ya Mpanda.

Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Katavi, Peter Nyakunga akielezea mafanikio ya ushirika kwa kipindi cha serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt Samia amesema Ushirika utendelea kuajiri watendaji wenye taaluma ili kuongeza tija na ufanisi kwa ajili ya kuimarisha zaidi usimamizi wa kila siku kwa masirahi ya vyama vyao.

Pamoja na hayo amesema wataendelea kuimarisha mifumo ya uthibiti kwa kuanzisha kamati mbalimbali na mifumo ya ukaguzi wa ndani kwenye vyama vya Ushirika.

Nyakunga amewaomba viongozi wa vyama vya Ushirika kujiepusha na vitendo vya rushwa na ufujaji wa fedha za Ushirika kwani huathiri nguvu ya wakulima na miongoni mwao kuteteleka kiuchumi.

Shabani Juma, Mkazi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo ambaye ni mwanachama wa Ushirika ameipongeza serikali kwa kazi nzuri ya kuimarisha sekta ya kilimo kwa kuhakikisha ruzuku inamfikia mkulima moja kwa moja bila kupitia kwenye Ushirika.

Mwanachama huyo licha ya pongezi hizo ameiomba serikali kuendelea kuhakikisha suala la mbolea kwa wakulima zinawafikia kwa haraka ili kuongeza uzalishaji kwenye kilimo.