Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya
VYAMA vya siasa Wilaya ya Mbeya kwa pamoja vimeafiki namna ambavyo mchakato wa maboresho ya Mpango Mkakati wa miaka mitano(2024/25 – 2029/30) wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya unavyofanyiwa kazi kwa kushirikisha wadau mbalimbali.
Akizungumza kwenye kikao cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya ya Mbeya(DCC) Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Jimbo la Mbeya Mjini ,Persi Mapunda amesema kilichofanywa na Serikali ya Wilaya ni jambo muhimu kwa kuwashirikisha kwasababu wao ndio wanaowawakilisha wananchi kupitia vyama vyao wanavyoviongoza.
Katibu huyo wa Chadema ameongeza kuwa Mapunda amesema kuwa watumishi na wapiga kura wao ndio wenye Mbeya hivyo ushirikishwaji ni lazima na muhimu kama kamati ya ushauri ya Wilaya ilivyofanya ili kupata maoni na kufikia malengo ya kuboresha Mpango Mkakati wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya.
Kwa upande wake katibu wa Chama cha Wananchi (CUF) Mbeya Mjini,Ibrahim Mwamkwama amesema, wameridhishwa na ushirikishwaji katika kuhakikisha Mbeya ijayo inakuwa bora kwa mwananchi mmoja mmoja na jamii kwa ujumla, hasa kwa kuboresha mpango wa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji, inayoelekezwa kwa Wanawake,Vijana na Watu wenye Ulemavu.
Kwa upande wake katibu wa chama cha ACT-Wazalendo Mbeya Mjini,Gift Almas amepongeza uendeshwaji wa zoezi la maboresho la mpango Mkakati tangu kuanza kwake kwa kuwashirikisha wananchi,viongozi wa kimila, wafanyabiasha, madiwani na viongozi wa vyama vya siasa, kwa kufanya hivyo Kamati ya Ushauri ya Wilaya imezingatia mambo muhimu kuelekea kuipata Mbeya yenye kukua na kuendelea kiuchumi, kisiasa na nyanja nyingine muhimu za kimaendeleo.
Pamoja na hayo Katibu huyo wa ACT-Wazalendo amewaasa wakazi wa Jiji la Mbeya na Wilaya kwa ujumla kujitokeza kwa wingi wakati litakapoanza zoezi la kuboresha Daftari la Kudumu la Mpiga Kura ili kujiweka tayari kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa Mwaka huu na Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka 2025.
Akimwakilisha Mwenyekiti wa Kikao cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya ya Mbeya,Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya Dormohamed Issa amewapongeza wadau kwa kushiriki vyema kikao hicho na kuwahimiza kuendelea kuwasilisha maoni yao kwa kamati husika ili kuijenga Mbeya kwa pamoja.
Kamati ya Ushauri ya Wilaya ya Mbeya(DCC) inayoongozwa na Mkuu wa Wilaya,Beno Malisa inaendelea kukusanya maoni ya wadau mbalimbali ili kukamilisha maboresho ya mpango mkakati wa miaka mitano wa Halmshauri ya Jiji la Mbeya. Unaotarajiwa kuanza kutekelezwa ifikapo Julai 2024.
More Stories
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi
Mbunge Ndingo:CCM imejidhatiti kuwaletea maendeleo wananchi