November 16, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Vyama vya siasa vyalaani ukiukwani wa maadili

Na Bakari Lulela, TimesMajira Online

VYAMA vya Siasa nchini vimekutana kulaani vikali vitendo vya ukiukwaji wa sheria na maadili ya Uchaguzi unaofanywa na baadhi ya vyama vya siasa katika uendeshaji wa mikutano yake ya kampeni.

Akitoa ufafanuzi dhidi ya ukiukwaji huo mgombea urais kupitia Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), Queen Cuthbert amesema, mara kwa mara wagombea wa baadhi ya vyama wamekuwa wakitumia lugha zisizofaa ikiwemo matusi na kejeli katika uendeshaji wa mikutano yao jambo ambalo linakwenda kinyume na taratibu za uchaguzi.

“Tumebakiza siku 39 za mikutano ya kampeni tunaviomba vyombo husika vinavyosimamia haki na sheria za Uchaguzi kukemea suala linalopelekea kutumia lugha zisizo za mantiki katika nchi na Taifa kwa ujumla ,” amesema Queen.

Kupitia suala hilo, wameiomba Tume ya Taifa ya Uchaguzi sambamba na vyombo vya usalama kukemea ukiukwaji huo ambao tafasiri yake ni kuchochea na kuvuruga amani ya watanzania ambayo imeota mizizi toka enzi.

Kwa upande wake, mgombea Urais kupitia Chama cha Demokratic Makini, Sesilia Mmanga amesema inatakiwa kama chama kiweze kujipambanua kwa sera madhubuti zenye mashiko ili wapiga kura waweze kuchagua mgombea bora atakae kuwa kivutio katika kinyang’anyiro cha Uchaguzi Oktoba 28 mwaka huu.