January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Vyama vya siasa vyaahidi ushirikiano na serikali

Na Mwandishi Wetu,Timesmajira, Online

VYAMA vya siasa nchini vimeahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, ambazo zinaongozwa na Rais, Samia Suluhu Hassan na Dkt. Hussen Ally Mwinyi.

Ahadi hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, John Shibuda kupitia taarifa yake akitoa maazimio ya kikao cha Kamati ya Uongozi ya Baraza hilo kilichakaa Juni 3 mwaka huu Jijini Dar es Salaam.

“Kamati kwa niaba ya vyama vyote vya siasa vyenye usajili wa kudumu ambavyo kimsingi vyote ni Wajumbe wa Baraza la Vyama vya Siasa, iliahidi kushirikiana na serikali zote mbili, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuleta maendeleo ya Watanzania,” imesomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Kamati ya Uongozi imemshukuru Rais, Samia Hassan Suluhu kwa uamuzi wake wa kutaka kukutana na viongozi wa vyama vya siasa nchini.

Katika hatua nyingine, Kamati ya Uongozi wa Baraza la Vyama vya Siasa kwa pamoja imeazimia kutoa pongezi kwa Rais Samia kwa kuwa Rais wa Awamu ya sita na Rais Mwinyi kwa kuwa Rais wa Zanzibar wa awamu ya nane, kutokana na ushindi alioupata katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Baraza hilo limeendelea kutoa pongezi kwa Rais Samia na Dkt. Mwinyi kwa namna wanavyoendesha serikali kwa kushirikisha vyama vya upinzani, ambapo taarifa hiyo imeeleza kuwa hiyo ni ishara ya kudumisha demokrasia ya vyama vingi hapa nchini.

Baraza la Vyama vya Siasa ni chombo kinachoundwa chini ya kifungu 21B cha Sheria ya Marekebisho ya Vyama vya Siasa namba 7 ya Mwaka 2009, ambalo linashirikisha wajumbe wawili ambao ni viongozi wa kitaifa kutoka vyama vyote 19 vyenye usajili wa kudumu, huku shughuli zake zikiratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.