September 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Vitongoji 90 ndani ya majimbo sita ya Mkoa wa Songwe kunufaika na umeme wa REA

Na Moses Ng’wat, Songwe.

SERIKALI imetoa kiasi cha shilingi Bilioni 10.84 kwa ajili ya mradi wa kusambaza umeme kwenye vitongoji 90 vya majimbo sita ya Mkoa wa Songwe ambapo jumla ya wananchi 2700 wataunganishwa na huduma hiyo .

Hayo yamebainishwa Septemba 26, 2024 na
Mhandisi Herini Mhina kutoka Wakala wa Nishati vijijini (REA) Makao Makuu, wakati wa hafla fupi ya kumtambulisha kwa Mkuu wa Mkoa Mkandarasi wa kampuni ya China Railway Construction Electrification Bureau Group Co. Ltd kutoka Nchini China atakayetekeleza mradi huo.

Mhina amesema mkataba wa utekelezaji mradi huo wa miaka miwili ulisainiwa Agosti 20,2024 na mkandarasi huyo kutoka China, ambapo utasimamiwa na REA na TANESCO ili kuhakikisha unatekelezwa kwa viwango huku kila kitongoji kilichopo kwenye mpango huo kinanufaika kama ilivyokusudiwa.

“Mradi huu utakua na laini ndogo ya kilomita 180 ambapo wateja watakuwa 2700 hivyo tunaahidi kuwa tutamsimamia mkandarasi amalize kazi ndani ya mkataba ili wananchi wanufaike na mradi,” amesema Mhandisi Mhina.

Kw upande wake Kaimu Meneja wa shirika la Umeme Tanesco Mkoa wa Songwe Mhandisi, Leonard Mtangi, amesema wamejipanga kuusimamia kw ubora mradi huo ili ukamilike kwa viwango vinavyotakiwa huku wananchi wakitakiwa kupisha maeneo ili wapate mradi.

“Huu utakuwa ni mradi wa sita wa umeme kutekelezwa mkoani hapa ambapo miongoni mwake ni mradi wa REA 3 awamu ya pili umevifikia vitongoji 127 vyote vina umeme na umefikia asilimia 90 kukamilika, mradi wa umeme jazilizi, mradi wa vitongojini,” amebainisha Mhandisi Mtangi.

Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo, amesema tayari vijiji vyote 307 vilishapatiwa huduma ya umeme na kwamba vitongoji 749 navyo tayari vimewashwa kati ya vitongoji 1489.

“Tunamshukuru Raisi Samia Suluhu Hassan kutuletea fedha hizi kiasi cha shilingi Bilioni 10.84 na leo tunamtambulisha mkandarasi ambaye atapanua wigo wa kuwafikishia wananchi kwenye vitongoji 90 kwenye majimbo ya mkoa huo, ambapo kila jimbo vitongoji 15 vitanufaika na kusaidia vitongoji 740 vya mkoa huo vyote vinafikiwa”.

“Niwaombe ndugu zangu REA na TANESCO msimamieni mkandarasi huyu afanye kazi kwa ubora kwani lengo la serikali kutoa fedha hizo ni kuhakisha huduma ya nishati inawafikiwa wananchi ambao wanauhitaji na huduma hiyo,” amesisitiza Chongolo.

Mradi huo utanufaisha vitongoji 15 katika majibo yote ya mkoa wa Songwe ambayo ni Ileje, Momba, Tunduma,Mbozi,Vwawa na Songwe.