Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
SERIKALI imetoa kiasi cha sh bil 6.5 kwa ajili ya kufikisha huduma ya nishati ya umeme katika viongoji 46 vilivyoko pembezoni mwa Miji ya Manispaa ya Tabora na Wilaya ya Nzega.
Akitambulisha mradi huo juzi mbele ya Mkuu wa Mkoa huo Balozi Dkt Batilda Burian, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Yusuph Ismail alisema mradi huo ni maalumu kwa ajili ya maeneo yaliyo pembezoni mwa miji tu.
Alisema mradi huo utatekelezwa katika Mikoa 8 hapa nchini ambapo kwa Mkoa wa Tabora utatekelezwa katika wilaya 2 tu za Tabora Manispaa na Nzega Mji ambapo jumla ya wateja 2,433 wanatarajiwa kuunganishiwa huduma hiyo.
Alitaja Mikoa mingine itakayonufaika na mradi huo wa usambazaji nishati ya umeme pembezoni mwa Miji kuwa ni Kagera, Geita, Singida, Tanga, Mbeya, Mtwara na Kigoma na Tabora yenyewe.
Alimweleza Mkuu wa Mkoa kuwa mradi huo unatekelezwa na Wakala wa Nishati Vijiji (REA) na utafikishwa katika vitongoji 27 vya manispaa Tabora na 19 vya Wilaya ya Nzega Mji.
Mhandisi Ismail alisema mradi huo utajenga jumla ya km 48.5 za mfumo wa umeme wa msongo wa kati na km 92 za msongo mdogo na watafunga mashine umba (Transfomer) 46 katika vitongoji vilivyobainishwa.
Alibainsiha kuwa Kampuni ya OK Electrical and Electronics Services Ltd ya jijini Dar es salaam ndiyo imepewa kazi ya kutekeleza mradi huo Mkoani Tabora na tayari wamesaini kandarasi hiyo.
Kwa upande wake Balozi Dkt. Batilda aliwataka wananchi wanaoishi katika maeneo yatakayopelekewa huduma hiyo kuchangamkie fursa hiyo kwa kuanza kufanya wayaringi katika nyumba zao ili kuunganishiwa nishati hiyo kwa gharama ndogo tu ya Sh.27,000.
‘Mradi huu ni muhimu sana kwa kuwa utabadilisha uchumi wa wananchi, watautumia kuanzisha viwanda vidogo na shughuli zingine za uzalishajimali ambazo zitawaingizia kipato hivyo kuinuka kiuchumi’, alisema.
Alimtaka Mkandarasi wa mradi huo kukamilisha kazi hiyo kwa wakati, mkataba wake ni miezi 18, na kuongeza kuwa hakuna sababu ya kuchelewa mradi huo wakati ana kila kitu kinachotakiwa kwa kazi hiyo.Aidha alimtaka kutoa nafasi za ajira kwa wakazi wa maeneo husika na kuwapa mshahara wao kwa wakati ili kuondoa malumbano yasiyo na tija.
Mbunge wa jimbo la Tabora Mjini Emanuel Mwakasaka aliishukuru Serikali ya awamu ya 6 kwa juhudi kubwa inazofanya ili kumaliza kilio cha umeme kwa wananchi.
Aliahidi kuwa wataendelea kumpa ushirikiano unaotakiwa ili kuhakikisha miradi yote anayoanzisha inakamilika kama ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inavyoelekeza.
Mkurugenzi wa Kampuni inayotekeleza mradi huo Mrisho Masudi aliahidi kutekeleza kazi hiyo kwa weledi na ufanisi mkubwa na kumaliza kabla ya muda uliowekwa.
Uzinduzi wa mradi huo kwa Mkoa wa Tabora umefanyika juzi katika kitongoji cha Mguluko, kijiji cha Itaga, kata ya Misha katika Manispaa ya Tabora.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba