Na Judith Ferdinand,TimesMajira,Online Mwanza
LICHA ya jitihada za Serikali na wadau wengine za kupigania haki za mtoto pamoja na kufanyika maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika kila mwaka, bado vitendo vya ukatili vinaendelea kwa watoto.
Akizungumza na Majira jijini Mwanza Ofisa Watoto Shirika la Mtandao wa Vijana na Watoto Mwanza (MYCN) Agness Michael,amesema shirika lao limejikita kupambana na kulinda haki za mtoto katika kulinda usalama na namna anavyokuwa kimwili na kiakili.
Licha ya jitihada hizo wanazochukua wao, Serikali na wadau wengine vitendo vya ukatili bado vimekuwepo kwa watoto,ambapo changamoto wanayokutana nayo zaidi ni kuwa jamii bado haijakubali kupigania na kutetea haki za mtoto.
Agness amesema,jamii yenyewe ndio watu wa kwanza kukiuka haki za watoto, hivyo wito wake kwa jamii na wazazi wote waendelee kupambana kwa kusaidiana na wadau wengine na Serikali.
“Ni muhimu jamii,wazazi pamoja na Serikali kuungana na wadau wengine kupigania haki za watoto ili waweze kukua na baadae wawe vijana na wazazi bora.
Kwa kufanya hivyo tutakuwa na taifa lenye watu ambao wameweza kufanikiwa kwa kukua kimwili, kiakili na kiafya pia,”alisema Agness.
Amesema ili kutekeleza kwa vitendo agenda ya 2040, kwa Afrika inayolinda haki za mtoto aliyoa wito wadau, wazazi na viongozi wote wajikite zaidi katika matamanio kumi ambayo wameyaweka na yakifuatwa wanaamini haki za mtoto zitafuatwa vizuri.
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Shirika la Railway Children Afrika (RCA) Mkoa wa Mwanza, Mary Mushi, alisema ili kuhakikisha haki za mtoto zinalindwa shirika hilo limekuwa likiwaunganisha watoto ambao wanaishi na kufanyakazi mitaani na familia zao, huku vijana wakiwawezesha kupata stadi za maisha ili waweze kusaidia na kuwajibika katika familia zao.
Mary amesema kwa kipindi cha mwaka mmoja wameweza kurejesha watoto 146 kwenye familia zao na vijana 140 ambao wamewawezesha katika mafunzo mbalimbali na sasa wanajitegemea.
“Katika shughuli zetu tumejifunza kuwa mifarakano ya familia,ukatilii ndio inapelekea watoto kukimbilia mitaani kwa hiyo tunajitahidi kufanya kazi na kutoa huduma ya kisaikolojia pamoja na kuwawezesha kiuchumi,”amesema Mary.
More Stories
Watakaokwamisha mapato Kaliua kukiona cha moto
Dkt.Gwajima aagiza kuundwa kamati za ulinzi wa watoto
Kilo 673.2,dawa za kulevya zakamatwa Bahari ya Hindi