Na Hadija Bagasha, TimesMajira Online, Tanga
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga Zahra Msangi amewataka viongozi wa Wilaya hiyo kuwa na moyo wa kujitolea wa kuendeleza miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na wafadhili baada ya muda wao kuisha ili kujenga imani kwa wafadhili wanaopeleka miradi kwenye maeneo yao.
Kauli hiyo ameitoa wakati wa kikao cha wadau wa maendeleo wa utekelezaji wa miradi ya World Vision Mkinga (AP) kilichoambatana na ziara ya kutembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa na shirika hilo kwenye jamii.
Mkurugenzi Zahra amewataka viongozi hao kuwa na moyo wa kujitolea na kuibeba miradi inayotelezwa na wafadhili kama ni ya kwao na waone kuwa wana wajibu wa kusimamia ili iweze kufika mbali.
“Kama tutaendelea kuona hivi vitu ni vya world vision au vya Mkurugenzi sababu mara nyingi mmekuwa mkifikiri Halmashauri ni hii ofisi halmashauri maana yake ni hizi mamlaka za serikali za mitaa kwahiyo kuanzia pale chini kwenye ngazi ya kitongoji kila mtu ana wajibu wa kufanya kazi ili kuona Halmashauri yetu inakwenda mbali, “alibainisha Mkurugenzi Zahra.
Aliongeza kuwa jamii bado hatujaihamasisha tutimie fursa hii kuihamasisha jamii inayotuzunguka kuwa na moyo wa kujitolea mara nyingi sana nimekuwa nikisema mimi kule kwetu Usangi suala la kujitolea watu wanaweza kuamua kulima hata mwamba na wakatengeneza barabara lakini kidogo huku kwetu Mkinga imekuwa tofauti wananchi hawapo tayari kujitolea wapo tayari kusema serikali haijafanya. Alisema Mkurugenzi Zahra.
Akizungumza katika kikao hicho, kaimu meneja wa shirika la world vision kanda ya Mashariki Daniel Chuma amesema kuwa bado jamii haijaona umuhimu wa miradi inayojengwa na wafadhili na kuiona kama ni mali yao kutokana na inapokabidhiwa kwao wanakuwa hawaitunzi ili itumike kwa kipindi kirefu.
Chuma amesema kuwa shirika hilo limekuwa likifanya miradi mingi kea kushirikiana na jamii pamoja na serikali ambapo ameishukuru serikali kwa ushirikiano mkubwa ambao imekuwa ikiwapatia katika ukamilishaji wa miradi hiyo ya kimakakati ambayo imekuwa ikibadilisha maisha ya wananchi.
“Kuna mafanikio makubwa katika miradi yetu lakini kuna mingine ina changamoto hivyo tunatamani serikali iingilie kati kutokana na miradi tuliyoitekeleza kipinfi cha nyuma kuwa na utunzaji mdogo na hatimaye kusababisha athari kwa wananchi, “alisisitiza Chuma.
Alisema jamii zinapaswa kuelimishwa ya kwamba miradi hiyo ni ya kwako hivyo wanajukumu la kuchangia gharama ndogo ndogo ili miradi hiyo iwe endelevu.
“Haifurahishi sana miradi tunapokabidhi mizuri lakini uendelevu wake unakuwa na mashaka kidogo rai yetu kwa pande zote zinazohusika ikiwemo serikali, jamii na sisi wadau wengine wa maendeleo hebu tuitazame kwa namna tofauti miradi hii ambayo imekamilika tuhakikishe inadumu kwa kufanya wajibu wetu ili jamii ya sasa na baadae ifanye kazi ya kutoa huduma kama ilivyokusudiwa, “alisema Chuma.
Kwa upande wake meneja wa world vision miradi ya Wilaya ya Mkinga (AP) Evodia Chija amesema kuwa kwa mwaka huu wametekeleza miradi mikubwa ya zaidi ya shilingi milioni 970 kwajili ya kuwajengea watoto madarasa ili waweze kupata elimu bora ikiwa ni pamoja na kuweka vyoo vya kisasa pamoja na kuhudumia watoto wenye mahitaji maalumu katika ujengaji wa madarasa.
Evodia ameishukuru serikali kwa kuweza kupambana na suala la mimba na ndoa za utotoni kwani hali ilivyokuwa hapo awali ni tofauti na hivi sasa.
Aidha Chija ameeleza kuwa miradi mbalimbali iliyoanza tangu mwaka 2010, wanaitekeleza katika kata saba za wilaya hiyo ambazo ni Manza, Doda, Mtimbwani, Boma, Parungu Kasera, Duga na kata ya Mkinga.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya Mkinga Amani Kisinya, alilishukuru shirika hilo kwa kutekeleza miradi mbalimbali katika wilaya hiyo hatua ambayo wanaunga mkono jitihada za Rais kuwaletea Maendeleo wananchi.
“Tunalipongeza shirika la World Vision kwa kusaidiana na mama, tunajua Rais anafanya mambo mengine kuwahudumia wananchi wake lakini pamoja na kazi kubwa anayoifanya lazima aaungwe mkono na wadau wengine wa Maendeleo kama wenzetu hawa wa World Vision kiukweli tunawashukuru na tunawaahidi tutaitunza miradi wanayotukabidhi,” alisema Mwenyekiti huyo.
Shirika hilo linatekeleza miradi yake katika wilaya za Kilindi, Handeni, Korogwe na Mkinga, na wameweza kutekeleza miradi yenye jumla ya shilingi bilioni 2 kwa mwaka huu.
Miradi wanayoitekeleza katika wilaya ya Mkinga ni pamoja na afya, elimu, maji, lishe, mazingira na masuala mtambuka yakiwemo ya jinsia.
More Stories
15 mbaroni tuhuma wizi wa shehena ya unga wa sembe
Wacheza rafu Uchaguzi Mkuu ujao waonywa
Hatua za kisheria kuchukuliwa kwa wanaohatarisha usalama Mbeya