Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
VIONGOZI wa umma Mkoani Tabora wametakiwa kutimiza wajibu wao kwa jamii kwa kufuata kanuni, taratibu na sheria zinazowaongoza na kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, uaminifu, uwazi, haki na kutopendelea.
Rai hiyo imetolewa juzi na Katibu Tawala wa Mkoa huo Dkt John Mboya alipokuwa akifungua Mafunzo ya siku moja kwa Viongozi na Watumishi wa umma kuhusu Sheria ya Maadili kwa Viongozi.
Alisema maadili ni suala muhimu si tu katika utumishi wa umma bali katika maisha yetu ya kila siku hivyo mafunzo hayo yatasaidia kuwajengea uwezo wa kufahamu zaidi sheria ya maadili ya viongozi wa umma Na 13 ya mwaka 1995.
Alibainisha kuwa viongozi wa umma ni kioo cha jamii hivyo wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, uaminifu, uwazi na haki pasipo upendeleo wowote na kuhakikisha rasilimali zilizopo zinatumika kwa maslahi ya jamii.
Aliwataka kuzingatia misingi iliyotajwa katika sheria ya maadili kwa viongozi na kutoa maamuzi ya haki ili kuimarisha misingi ya demokrasia na utawala bora.
Dkt Mboya alibainisha kuwa ukuzaji wa maadili kwa viongozi ni moja ya jitihada zinazofanywa na serikali ili kuhakikisha malengo ya Dira ya Taifa yanafikiwa kama yalivyopangwa.
Naye Katibu Msaidizi wa Idara ya Ukuzaji Maadili Sekretarieti ya Viongozi wa Umma kutoka Makao Makuu Fabian Pokela aliwataka kuwa makini katika utunzaji siri za serikali na kuwa na msimamo wa kutopokea zawadi kwa kiwango chochote kwani kinaweza kuwaletea matatizo.
Alisema wajibu wa sekretarieti ya maadili ya viongozi wa umma ni kuwaelimisha , kuwakumbusha na kuwasisitiza kutimiza wajibu wao ili wawe wasafi na kutotenda makosa yanayoweza kuwaletea matatizo.
Awali Katibu Tawala Msaidizi anayeshughulikia Rasilimali watu Mkoani hapa Daniel Balago alisema mafunzo hayo ni hatua muhimu kwa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma katika kusimamia na kukuza maadili nchini.
Mbali na kujaza fomu za maadili ya viongozi, alisema mafunzo hayo pia yanahusisha misingi mingine ikiwemo uadilifu, kuheshimu sheria, kujali watu wengine, uwazi, kujizuia na tamaa na kuepuka mgongano wa ki maslahi.
Mada zilizowasilishwa katika semina hiyo ni Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Uwajibikaji wa pamoja, Kanuni za Mgongano wa Maslahi, Kanuni za Ahadi ya Uadilifu kwa Viongozi wa Umma na Tamko la Rasilimali na Madeni.
More Stories
RC Chalamila awataka ndugu,Jamaa na marafiki kuwa wavumilivu zoezi la uokoaji likiendelea
Baraza la Madiwani lafukuza watumishi wawili idara ya afya
Wanasheria waombwa kusaidia kusimamia sheria, sera ulinzi wa taarifa