December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Viongozi wapya ACT-Wazalendo Songwe wapewa mtihani

Na Moses Ng’wat,Timesmajiraonline,Songwe.

NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Joran Bashange amewaagiza viongozi wa chama hicho mkoani humo kuhakikisha wanafikisha wanachama 76,000 kutoka 746 waliopo sasa.

Bashange ametoa agizo hilo leo Jumatano Januari 17, 2024 wakati akihutubia mkutano mkuu wa uchaguzi kwa ngazi ya mkoa uliofanyika katika ukumbi wa Mkonongo mjini Vwawa wilayani Mbozi.

Akizungumza katika mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu huyo Taifa amesema ili chama hicho kiweze kufanya vizuri katika chaguzi zinazokuja ukiwemo uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu wa wadiwani, wabunge na Rais ni lazima kila mkoa kuwa na mtaji wa wanachama.

“Nimeangalia kwenye database (kanzi data) Mkoa wa Songwe mpaka sasa una wanachama 746 tu, lazima viongozi wahakikishe wanashirikiana kutafuta wanachama ili kufikisha wanachama 76,000. Hili litatusaidia katika kuendesha chama na kufikia malengo yatu ya kuchukua dola ” amesema na kuongeza;

“Mkoa huu unatakiwa rangi ya zambarau itawale (rangi ya bendera ya chama hicho) kama tukifikisha wanachama 76,000 itakuwa rahisi kujiendesha na kuwa na uhakika katika nafasi za uchaguzi. Wenzetu Kigoma ukisema wanachama wa ACT-Wazalendo wanaonekana wana zaidi ya wanachama 30,000. Tunatakiwa tuongeze wanachama ili hata mikutano mikuu mingine tutafute eneo kubwa zaidi” ameeleza.

Pia, Naibu Katibu huyo amewataka wagombea ambao hawajachaguliwa katika nafasi mbalimbali kuwa wamoja ili kuendelea kukijenga chama badala ya kugawanyika.

“Viongozi mnatakiwa muwe kitu kimoja, msiwe na makundi…tunachagua mmoja ili tubaki wamoja na
Kazi yenu ikawe kutafuta wanachamakatika Mkoa wenu”

Msimamizi wa uchaguzi huo, Hussen Kaliango alimtangaza Dk Ali Msenda kuwa Mwenyekiti mpya wa Chama hicho Mkoa wa Songwe baada ya kupata kura 58 kati ya 72 huku akiwashinda wagombea wenzake wawili ambao ni Leniwa Mahenge aliyepata kura tat una Asukile Kabango ambaye naye alipata kura tatu huku Michael Nyilawila akitetea nafasi yake ya Katibu wa Mkoa ambaye amepata kura 53 akimshinda mgombea mwenzake Kelvin Mjwanga ambaye alipata kura 14.