December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Viongozi wa Umma watakiwa kuwasilisha tamko lao

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

SEKRETARIETI ya Maadili ya Viongozi wa Umma imewataka Viongozi wote wa Umma kuzingatia matakwa ya katiba na sheria ya Maadili kwa kuwasilisha tamko la Rasilimali na madeni ifikapo Disemba 31 mwaka huu. 

Imesema kuwa mwenendo wa uwasilishaji taarifa hizo hauridhishi kwani hadi kufikia Disemba 20,2023 ni Viongozi  2,475 pekee ndio wameweza kuwasilisha tamko lao kwa Kamishna wa Maadili kati ya Viongozi 15,762 sawa na asilimia 16 ya viongozi wote huku zikiwa zimebaki siku 10 kufika tarehe ya mwisho. 

Hayo yameelezwa jijini hapa leo Disemba 21,2023 na Katibu, Ukuzaji wa Maadili,Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma,Waziri Kipacha wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya urejeshaji wa tamko la rasilimali, madeni na mfumo wa ujazaji fomu za tamko kwa njia ya mtandao. 

“Idadi hii ni sawa na asilimia 16 ya viongozi wote wanaopaswa kuwasilisha tamko la Rasilimali na madeni kwa mujibu wa sheria, napenda kuchukua nafasi hii kuwaomba ambapo bado watimize wajibu wao ili kuungana na Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hasan, Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango na Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa ambao tayari wametimiza wajibu huo, “amesema

Aidha amewataka viongozi wengine ambao bado hawajawasilisha matamko yao wakiwemo waliotamkwa katika tangazo la serikali Na. 857 la Novemba 24,2023 kuwa tangu siku ya tangazo hilo wanawajibika kutimiza masharti yote ya sheria ya Maadili ya viongozi wa Umma. 

Kipacha ametaja taarifa zinazotakiwa kutumwa na viongozi ni pamoja na majina matatu, simu ya mkononi, barua pepe binafsi ya kiongozi husika, Taasisi anayofanyia kazi wadhifa wa kiongozi na tarehe ya uteuzi . 

Akizungumzia kuhusu viongozi wapya amesema watatatikiwa  kuwasilisha taarifa zao ndani ya siku 14 baada ya kuteuliwa au kupandishwa cheo ambapo watatumiwa taarifa za siri kwa ujumbe mfupi kupitia simu zao kuwezesha kuingia kwenye mfumo wa ODS.

“Kuhusu ujazaji fomu za tamko la Maadili kwa njia ya mtandao, Kipacha amesema Ofisi hiyo pia imeanza kutumia mfumo huo kuendana na mabadiliko ya sayansi na Teknolojia (ODS)kuwezesha viongozi ambao hawatapata muda wa kufika kwenye ofisi hizo kujaza kwa njia ya mtandao,”amesema.Â