Na Prosper Rutayuga, Timesmajira Online DSM
VIONGOZI wa dini ya Kiislamu waliopo mahabusu mbalimbali nchini wakikabiliwa na tuhuma za ugaidi, wamemuomba Rais Samia Suluhu Hassan, aingilie kati ili haki itendeke.
Akizungumza kwa niaba ya familia hizo, Habiba Hussein Msabile, 28 Januari 2023, jijini Dar es Salaam, amedai masheikh hao wamesota rumande kati ya miaka sita hadi 10, bila mashauri yao kusikilizwa mahakamani kwa maelezo kwamba Serikali haijakamilisha upelelezi wake.
“Tumeamua kupaza sauti kwa sababu Rais Samia amepata kutamka kwamba katika Serikali yake mtu hatakamatwa mpaka pale vyombo vya usalama vimepata ushahidi wa tuhuma dhidi yake. Amepata kutoa maelezo kuwa, katika Serikali yake raia waliowekwa magerezani kwa muda mrefu kwa hoja ya upande wa Serikali kutafuta ushahidi wataachiwa huru,” amedai Habiba.
Habiba amedai kuwa, wameamua kumwangukia Rais Samia baada ya jitihada zao za kuzungumza na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), kutozaa matunda.
“Tumekuwa tukienda katika mamlaka hiyo jijini Dar es Salaam na Dodoma mara kwa mara bila mafanikio. Kwa mara ya mwisho ofisi hiyo ilitupa majibu ya mdomo kuwa mpaka Julai 2022, ufumbuzi utapatikana ima kwa Serikali kupelekea ushahidi mahakamni au mashauri hayo kufutwa,”amedai Habiba.
Habiba amedai kuwa, masheikh hao 117 ni kati ya masheikh zaidi ya 180 waliokuwa wanakabiliwa na tuhuma za ugaidi ambao walikamatwa kati ya 2013 hadi 2017, ambapo hadi sasa DPP amewafutia mashtaka masheikh 69 ambao wako huru.
Naye Zubeda Rajab, amemuomba Rais Samia aingilie kati suala hilo kwa kuwa miongoni mwa watuhumiwa hao ni wazee walio na umri zaidi ya miaka 90 pamoja na watoto waliokamatwa ingali wako shule, kama dhamana ya wazazi wao waliokimbia wakati wa msako.
“Mfano kuna mzee Suleman Ulatrule Simba ana umri wa miaka 96 anashikiliwa gerezani miaka nane, zaidi ya hilo anashikiliwa gerezani yeye na familia yake ya watu sita na hakuna mtu wa kuwasaidia. Mfano mwingine kuna watoto waliokamatwa wakiwa na miaka 15 na 17, kwa madai kwamba walikusudia kuwakamata baba zao lakini hawakupatikana,”amedai Zubeda.
Mwaka 2021, Ofisi ya DPP iliwaacha huru baadhi ya masheikh waliosota gerezani kwa zaidi ya miaka sita, wakikabiliwa na mashtaka ya ugaidi, baada ya kuwafutia kesi zilizokuwa zinawakabili kwa kukosekana kwa ushahidi.
More Stories
TMDA:Toeni taarifa za ufuatiliaji usalama wa vifaa tiba ,vitendanishi
The Desk & Chair yashusha neema Gereza la Butimba
TVLA,yapongezwa kwa kuzalisha chanjo