October 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Viongozi wa dini wasisitiza amani

Na Waandishi Wetu,TimesMajira Online,mikoani

WANASIASA wametakiwa kulinda amani na utulivu ambao Mungu ameijalia nchi ili iendelee kuwepo katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi kwani itakuwa ni makosa makubwa kuhamasisha vijana kuingiza taifa kwenye shida kubwa.

Aidha, wamewataka wasihamasishe wananchi kushiriki maandamano, kulinda kura kinyume cha sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Wito huo umetolewa kwa nyakati tofauti na viongozi wa dini mikoa ya Simiyu na Shinyanga juzi wakati wakizungumzia masuala mbalimbali kuelekea uchaguzi mkuu.

Mkoani Shinyanga wakazi wa mkoa huo wametahadharishwa kutokuunga mkono vitendo vyovyote vinavyoweza kuwa chanzo cha kutokea kwa uvunjifu wa hali ya amani.

Tahadhari hiyo ilitolewa na wajumbe wa Kamati ya Amani ya Mkoa wa Shinyanga ambao wamewataka wananchi wote wenye kuthamini amani kutokubali kutumiwa na wanasiasa wakati huu wa kipindi cha uchaguzi hasa siku ya upigaji kura.

Akitoa taarifa ya kamati hiyo kwa waandishi wa habari, Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Amani mkoani humo, Sheikh Khalfan Ally amesema kila Mtanzania ana wajibu wa kuhakikisha analinda amani iliyopo nchini kwa vile iwapo itatoweka haitokuwa rahisi kuirejesha.

Sheikh Ally amesema iwapo amani itatoweka wahanga wakubwa watakuwa ni wanawake, wazee na watoto hasa wale wenye mahitaji maalumu miongoni mwa jamii.

“Kamati ya Amani ya Mkoa wa Shinyanga inatoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Shinyanga na Taifa kwa ujumla kutokubali kutumiwa na wanasiasa wakati huu wa kipindi cha uchaguzi hasa siku ya upigaji kura Oktoba 28, mwaka huu,” amesema Sheikh Ally na kuongeza;

“Tunawasihi wazazi na walezi wa familia nchini kote kujiepusha na kushawishiwa kushiriki maandamano, fujo, na vurugu zozote wakati wa uchaguzi kwa kuwa matokeo yake watakabiliana na mkono wa sheria wakati wahamasishaji wa vurugu wakiikimbia nchi na kuwaacha wachache wakihangaika.”

Katika hatua nyingine Kamati hiyo imetoa rai kwa baadhi ya viongozi wa madhehebu ya kidini nchini wanaojitokeza kuhamasisha vijana kukaa kwenye vituo vya kupigia kura, waache tabia hiyo mara moja.

“Sisi Kamati ya Amani ya Mkoa wa Shinyanga, tunatoa wito na kuwaomba viongozi wote wa madhehebu ya kidini mkoani hapa na nchini kote kwa ujumla wajiepushe na vitendo vyovyote vyenye viashiria vya uvunjifu wa amani,” ameeleza Sheikh Ally.

Mkoani Simiyu, viongozi wa dini wamewataka Watanzania wote kutambua kwamba kuna maisha baada ya uchaguzi, hivyo hawana sababu ya kulewa amani iliyopo nchini, kwani kuna watu waliyoitengeneza wakiongozwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

“Nchi yetu ni tajiri sana na hakuna nchi ambayo ni tajiri haikodolewi macho ya husuda, uroho. Tuwe makini sana, mara nyingi watu hao huwa wanafanikiwa siku hizi za uchaguzi,” amesema mmoja wa viongozi hao.

Mmoja wa viongozi wa dini ya kiislamu akizungumza kwenye mkutano huo, amesema wao kama Waislamu hawana mgombea ambaye wamemtangaza kwamba anasimamia waislamu.

Aidha, kiongozi mwingine amesema; “siasa ni mabishano baina ya watu wanaogombania kitu kimoja kwa lengo la kuleta maendeleo ndani ya jamii.

Tunahitaji hiyo siasa sasa tuweze kufika mahali tunakubaliana kwamba tunahitaji amani. Hadi sasa siasa imefikia wapi? Bado hali haijawa mbaya, bali yapo majibizano ambayo wanazungumzia sasa kabla ya kufikia matokeo ya hayo majibizano,”amesema.

Kwa Simiyu, amesema hali haijawa mbaya, lakini sehemu mbalimbali wamesikia majibizano yakitokea. “Sisi tunasema busara iwe sehemu ya utendaji wetu, bila busara hatuwezi kumaliza suala la uchaguzi.

Kila mwanasiasa ajue kwamba busara yake ndiyo itakayonusuru taifa letu. Ubabe hautatusaidia, tunahitaji busara, ndiyo maana leo viongozi tupo hapa, tunajua tufanye nini ili amani yetu iendelee,”.