November 8, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Vikao vya Mashirikiano kuendelea kufanyika

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Serikali imedhamiria kuendeleza kufanya Vikao vya Mashirikiano ili kufanya tafakari ya pamoja juu ya shughuli zinazofanywa na Ofisi ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Ofisi ya Makamu wa pili wa Rais Zanzibar.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene katika mkutano wa kwanza wa Vikao vya Mashirikiano katika ngazi ya Mawaziri kilichofanyika Ukumbi wa Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale Kikwajuni Zanzibar.

“Kushirikiana huku hakuepukiki na kwa bahati nzuri serikali zote ni za Chama Cha Mapinduzi lazima tukutane mara kwa mara ili tuweze kutathimini ni namna gani tunatekeza ilani ya Uchaguzi”.

Hii ni hatua nzuri tumefikia na ni lazima tuboreshe ratiba zaidi, ili tuende zaidi ya kiwango tunachokwenda sasa, alisema Waziri.

“Tusiishie kukutana ngazi hii tuu,  tuweke utaratibu wa  uratibu wa kukutanisha makundi na hasa vijana ili waweze kuufahamu Muungano wetu na wauenzi ili uwe na faida iliyokusudiwa na waasisi wetu wa Nchi hizi Mbili”.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera Uratibu na Baraza la Wawakilishi Mhe. Hamza Hassan Juma amesema Muungano wetu ni wa kipekee na kuendelea kukutana hivi ni kuimarisha mawazo ya waasisi wetu wa Muungano.

“Tunakaa tunazungumza mambo ya Wizara na taasisi zetu lakini tunakumbushana umuhimu wa Muungano na umoja wetu”.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene akizungumza katika Kikao cha Mashirikiano kilichofanyika Mjini Zanzibar.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera Uratibu na Baraza la Wawakilishi Mhe. Hamza Hassan akizungumza katika Kikao cha Mashirikiano kilichofanyika Mjini Zanzibar
Watendaji wa Ofisi ya  Makamu wa Pili wa Rais, Sera Uratibu na Baraza la Wawakilishi  pamoja na Watendaji wa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu wakiwa katika kikao cha pamoja cha Mashirikiano.