Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Serikali imeruhusu vijiji 46 katika mkoa wa Simiyu vilivyokuwa katika mgogoro wa matumizi ya ardhi kwenye maeneo ya hifadhi kuendelea na shughuli za kibinadamu ambazo hazitaathiri shughuli za uhifadhi wa wanyama pori na ndani ya eneo kinga la mita 500.
Aidha, vijiji viwili kati ya 48 vya mkoa wa Simiyu vilivyokuwa katika mgogoro wa aina hiyo vinafanyiwa tathmini ili kumega eneo ndani ya hifadhi ya Jumuiya ya Jamii (WMA).
Vijiji 46 vilivyoruhusiwa ni vile vilinavyoendesha shughuli za kibinadamu kwenye eneo kinga la mita 500 linalotenganisha vijiji hivyo na hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Pori la Akiba la Maswa pamoja na pori la akiba la Kijereshi.
Hayo yamebainishwa tarehe 17 Oktoba 2022 mkoani Simiyu na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Angeline Mabula katika kikao baina ya Kamati ya Mawaziri nane wa Wizara za Kisekta na viongozi wa mkoa na wilaya kupeleka mrejesho wa Baraza la Mawaziri kuhusiana na utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975.
Kwa mujibu wa Dkt. Mabula ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo, pamoja na uamuzi huo wa serikali uliotolewa mkoa utakuwa na jukumu la kusimamia utekelezaji wa maamuzi hayo kwa kushirikiana na taasisi na mamlaka zote zilizopo ndani ya mkoa.
“Kamati ya wataalamu inayojumuisha wataalamu kutoka ngazi ya taifa, mkoa, wilaya na taasisi zetu za uhifadhi ilianza kazi za tathmini katika vijiji husika mwezi septemba 2022” alisema Dkt Mabula.
Dkt. Mabula aliongeza kuwa, tathmini iliyofanyika inahusisha kufanya vikao na viongozi wa serikali za vijiji na kuembelea eneo la kinga la mita mia tano kubaini matumizi yaliyopo sasa.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, Khamis Hamza Chillo akizungumza katika kikao hicho alisisitiza suala la elimu ya sheria ya utunzaji mazingira na vyanzo vya maji ili kuepuka uharibifu unaoweza kufanywa na binadamu.
Naye Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde alieleza nia ya Wizara yake kutungwa kwa sheria ya kilimo ili kulinda ardhi ya kilimo kwa lengo la kuboresha sekta hiyo nchini.
Baadhi ya Mapendekezo ya kamati ya Mawaziri wa Wizara za Kisekta kuhusiana na utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi ni pamoja na kubakisha vijiji na vitongoji vilivyomo ndani ya hifadhi, kubainisha maeneo ya hifadhi yaliyopoteza sifa ili kugawiwa kwa wananchi sambamba na kuhakiki na kurekebisha mipaka kati ya hifadhi za misitu, wanyama na makazi.
Pia yapo mapendekezo ya kumega baadhi ya hifadhi na kugawia wafugaji na wakulima, kufanya mapitio ya sheria zinazohusiana na matumizi ya ardhi, kupitia upya sheria ya vyanzo vya maji inayozungumzia mita 60 na kufutwa kwa mashamba yasiyoendelezwa.
More Stories
Wasanii wa ‘Comedy’ kuwania tuzo
Wazazi wa Wanafunzi Sekondari ya Muhoji waamua kutoa chakula kwa watoto wao
Jokate achangia milioni 3 mfuko wa bodaboda