November 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Vijana watakiwa kutotumika katika vitendo vya kihalifu,uvunjifu wa amani

Na Mwandishi wetu, timesmajira

Vijana katika nchi zinazozungukwa na maziwa makuu wamewataka
kuacha kutumika katika vitendo vya uhalifu na uvunjifu wa amani ambavyo kwa kiasi kikubwa vina athari kwao na nchi zao kwa ujumla.

Akizungumza Jana jijini Dar es Salaam ,Naibu Meya wa Jiji la Dar es Salaam Ojambi Masaburi wakati akipokea matembezi ya kuadhimisha siku ya amani dunia yaliyofanywa na vijana kutoka nchi za maziwa makuu ambazo ni Demokrasia ya Congo(DRC), Uganda, Tanzania, Rwanda na Burundi.

Masaburi amesema ni muhimu vijana kuacha kushabikia mambo yasiyokuwa ya msingi ambayo yanaweza kuleta machafuko na uvunjifu wa amani huku akiwataka wayasema yale mema ya serikali na kutoa ushauri pale unapohitajika kufanya hivyo.

“Bila kuwa na amani hatuwezi kuwa na maendeleo, amani inapotea tunapoteza ndugu, baba, mama na watoto pamoja na watu wenye mahitaji maalum kwa maana ya walemavu,” amesema Masaburi na kuongeza

“Kwa mujibu wa takwimu za dunia zinaonesha kuwa zaidi ya vijana Bilioni 1.4 duniani wanaishi katika maeneo au nchi zenye mchafuko na wanawake 600,000 ambao nao wanaishi kwenye nchi zenye machafuko, hizi zi takwimu nzuri,” amesema

Naye Ofisa Maendeleo ya Vijana wa jiji la Dar es Salaam, Happness Joackim amesema kupitia maadhimisho hayo wanawahimiza vijana hususani waliopo katika nchi ambazo zinazungukwa na maziwa makuu kulinda na kutunza amani za nchi zao.

Amesema vijana wasikubali kujiingiza katika machafuko ya kikabila, kisiasa au ya nchi na nchi kwa sababu kuingia katika migogoro hiyo kutaleta matatizo mengi ikiwemo kupoteza ndugu, jamaa na marafiki huku kundi kubwa linaloathirika ni watoto, wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Kwa upande wake Mratibu wa Taifa wa Mtandao wa vijana wa nchi za maziwa makuu kuhusu Amani na Utulivu .Jimmy Luhende amesema kongamano hilo la siku tatu limeweza kuwakusanya vijana hao na kujadili mambo mbalimbali ikiwemo kupanga mijadala ya kumaliza migogoro mbalimbali katika nchi zao na kudumisha amani.

Amesema tofauti zinapotokea ikiwemo kupeleka majeshi,kutunishiana misuli katika nchi hizo za maziwa makuu haziwezi kuleta amani na wala kuwa suluhisho.

Aidha Katibu wa Asasi ya Vijana Youth VDT,Nicholus Luhende amesema kwa mara ya kwanza kuanza kwa kongamano hilo lilianza nchini Congo,Kigali,Uganda na sasa Tanzania lengo ikiwa ni kuwakutanisha vijana kutoka nchi hizo kujadili masuala ya amani.

”Nchi ambazo zinatuzunguka Tanzania zimekuwa na changamoto mbalimbali katika masuala ya amani hivyo kongamano hili limetupa nafasi ya kukaa pamoja na kujadili kwani kupitia maongezi itaweza kutatua matatizo yaliyopo,”amesema.