November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Vijana watakiwa kuchangamkie fursa za scholarship nje ya nchi

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah (kulia) akimsikiliza Mkurugenzi wa Global Education Link, Abdulmalick Mollel,  kwenye maonyesho ya  vyuo vikuu yaliyoanza jana na yanayoendelea visiwani Zanzibar kutoka kwa mmoja wa washiriki hao.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah (kulia) pamoja na Mkurugenzi wa Global Education Link, Abdulmalick Mollel,  kwenye maonyesho ya  vyuo vikuu yaliyoanza jana na yanayoendelea visiwani Zanzibar kutoka kwa mmoja wa washiriki hao.

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

WAKALA wa Elimu ya Vyuo Vikuu nje ya Nchi Global Education Link (GEL), imeanza kudahili wanafunzi papo hapo kwenye maonyesho yanayoendelea kwenye viwanja vya Maisala visiwani Zanzibar.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa GEL, Abdulimalick Mollel, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maonyesho hayo yanayoendelea visiwani humo yaliyoanza tarehe 15 mpaka 21.

Pia alizungumzia maonyesho  yaliyoandaliwa na Globali Education Link yatakayofanyika katika hoteli ya Johari Rotana kuanzia tarehe 23 na 24 jijini Dar es Salaam na vyuo vikuu vingi vya nje kutoka India, China, Urusi, Irani, Uingereza, Canada, Australia na vingine vya mataifa mbalimbali.

Alisema kwenye maonyesho hayo kuna vyuo vya nje ya nchi ambavyo vimetoa udhamini wa asilimia 50 kwa wanafunzi wanaotaka kwenda kusoma kwenye vyuo hivyo na vingine vimetoa ufadhili wa asilimia 100.

“Tumeleta wawakilishi wa vyuo 20 kutoka Irani kuna ufadhili wa asilimia 100 analipiwa kila kitu na kuna vyuo ambavyo mwanafunzi atalipiwa asilimia 50 ya ada kwa hiyo mwanafunzi akija kwenye maonyesho haya akichagua kozi GEL tunamdahili hapahapa,” alisema

Alisema lingine la manufaa kwenye maonyesho hayo ni uhusiano wa vyuo vikuu vya ndani na nje ya nchi kwani uzoefu unaonyesha kuwa asilimia kubwa ya wahitimu wa vyuo vya nje ya nchi wanaajiriwa mara tu wanapomaliza vyuo.

Alisema mara nyingi wanafunzi wanaohitimu vyuo vya hapa nchini huanza kuhangaika kutafuta ajira kwenye maeneo mbalimbali na kulalamikia ugumu wa ajira wakati vyuo vya nje hali ni tofauti kwa wahitimu wao.

“Vyuo vya nje vinafanikiwa kutoa wahitimu ambao wanaajiriwa mara tu wanapohitimu ndiyo maana tumewakutanisha na vyuo vya ndani ili waweze kubadilishana maarifa, wao wanafanyaje kuwaaandaa wanafunzi tunaangalia je ni suala la mitaala au ushirikiano mwema na taasisi za ajira,” alisema

“Kwa hiyo tulicholeta hapa ni ushirikiano baina ya vyuo hivi kama kuna chuo kikuu cha hapa ndani kilichoko tayari kushirikiana na chuo chochote cha nje watakutana na kubadilishana ujuzi na maarifa mbalimbali ili waweze kutoa wahitimu bora,” alisema

Alisema lingine ni fursa ya kupata udahili kwani baadhi yao wamekuwa wakikosa nafasi za kujiunga na vyuo vikuu kutokana na ufinyu wa nafasi kwenye baadhi ya kozi wanazoomba hasa zile za afya na uhandisi.

Mollel alisema idadi ya wanafunzi wanaoomba nafasi za kozi za afya na uhandisi ni wengi kuliko nafasi zilizopo hivyo kuna umuhimu wa kuwatafutia nafasi kwenye vyuo mbalimbali nje ya nchi.

“Tumekuja na vyuo hapa ambavyo vinaruhusu wanafunzi kudahiliwa hapa nchini akasoma kwenye chuo cha nje kwa miaka kadhaa kisha akarudi kumalizia elimu yake hapa Tanzania kwa hiyo sisi tunaona hii ni fursa kwa vijana wetu,” alisema.

Aidha, alitoa wito kwa wanafunzi wa Zanzibar na wadau wa elimu kuwa dunia imekuwa kama kijiji hivyo wanatakiwa kutumia fursa za nje kwani hata gharama za masomo kwenye vyuo vya nje zinalingana na za masomo ya hapa nchini.

“Watanzania wachangamkie fursa za ufadhili wa vyuo vikuu wasidharau kwasababu tuna mtindo wa wa kudharau kwasababu ya kuogopa kujaza fomu zenye maelezo mengi lakini sisi tuna ofisi hapa Zanzibar waje tutawatafsiria maelezo hayo,”

“Unaweza kukuta fomu moja ya scholarship inakaratasi hadi 13 sasa kwa mwanafunzi ni mara yake ya kwanza kuomba ufadhili anakata tama lakini kwa kuwa tuko hapa waje tuwaelekeze na tuko hapa kufungua fursa zilizoko duniani ili wanafunzi waweze kusoma nje,” alisema

Aliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Dk. Hussein Mwinyi kwa kuonyesha utayari wa kushirikiana na Global Education Link kuendelea kuwatafutia fursa za elimu ya juu nje ya nchi.