October 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Vijana wahimizwa kujiunga na BBT

Na Mwandishi wetu, Timesmajira

SERIKALI imeendelea kuhimiza makundi ya vijana wa kitanzania kujiunga katika Programu ya Kujenga,Kesho Bora ( BBT) ili waweze kunufaika na fursa mbalimbali zitolewazo hususan katika Sekta ya kilimo .

Hayo yameelezwa jijini Dar es salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo,Gerald Nyeri katika Mkutano Maalum wa Taasisi inayojitolea kuweka Wakulima Wadogo katika Kitovu cha Uchumi Barani Afrika (AGRA) uliowashirikisha wadau mbalimbali wa kilimo.

Amesema Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inawahimiza na kuwashauri vijana kujiingiza katika fursa mbalimbali za kimaendeleo.

“Serikali ipo tayari kuyashirikisha makundi ya vijana kutoka vyuo vikuu hususan wale walio katika sekta ya kilimo pamoja na wataalamu mbalimbali kushiriki katika kuendeleza sekta hiyo nchini,”amesema Nyeri

Aidha Nyeri amesema utekelezaji huo umekuja baada ya Rais Dkt.Samia kutoa mkazo katika suala hilo la Kilimo kupitia kwa mtangulizi wake Hayati John Magufuli kwa kulisisitiza na kulibariki ndipo likaundwa Shirika la AGRA ili vijana waweze kujishughulisha na masuala ya kilimo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Kilimo kutoka AGRA,Vianey Rweyendela amesema jumla ya vijana wote ni asilimia 65 wanaoshi vijijini hivyo ni bora kuanza na asilimia hiyo kwa kuwa wakazi wengi hususan vijana waweze kunufaika kirahisi kabisa.

Amesema shughuli za AGRA zinalenga makundi hayo kwa kuwa vijana ndio kundi kubwa, lenye uelewa, utayari na kujitoa katika kutekeleza masuala mbalimbali ndani ya jamii zao.

Nae mnufaika wa kwanza wa BBT kutoka Mkoa wa mbeya ambaye ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Mkami,Yussuph Telele amesema kupitia shirika la AGRA endapo litawawekea mifumo mizuri kwa wakulima itaweza kusaidia kukopeshwa mazao, mbegu, mbolea na madawa.