Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
JUMLA ya vijana 78 wa kike na kiume wamehitimu mafunzo ya umahiri katika fani mbali mbali zinazotolewa katika Chuo cha Ufundi Stadi VETA Mkoani hapa na kutunukiwa vyeti.
Miongoni mwa mafunzo waliyopata chuoni hapo ni uchomeleaji na uungaji vyuma, umeme wa magari, umeme wa majumbani, uashi, ufundi magari, uselemala, ukarabati wa bodi za magari uhazili na kompyuta.
Akizungumza katika mahafali hayo Asanterabi Kanza ambaye ni Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Magharibi aliwataka vijana wa jinsia zote kuchangamkia mafunzo hayo ili kupata fursa ya kujiajiri au kuajiriwa na kujiingizia kipato.
Alisema vijana wote wanaopitia VETA na kupata elimu ya ufundi stadi wanakuwa mahiri katika fani mbali mbali hivyo kuwa nguvu kazi ya kutegemewa kwa kuzingatia azma ya serikali ya awamu ya 6 ya kuwa nchi ya uchumi wa viwanda.
Akijibu changamoto zilizotolewa katika risala ya wahitimu hao Kanza alisema wamezipokea na kubainisha kuwa baadhi wameshaanza kuzifanyia kazi akitoa mfano wa suala la upungufu wa vitabu na viti.
Kuhusu uchakavu wa vyoo alisema tayari wameanza kufanyia ukarabati wa miundombinu yote ya chuo hicho na tayari wameagiza kompyuta 20 ili kuziba pengo la upungufu uliopo.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo hicho Dkt. Zebedayo Kyomo aliishukuru serikali ya awamu ya sita chini ya rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kukiongozea nguvu ili kuhakikisha kinaendelea kujiendesha.
Alibainisha kuwa Chuo hicho kilichoanzishwa mwaka 1999 kwa sasa kinakabiliwa na changamoto ya uchakavu wa mashine za kujifunzia pamoja na majengo ya karakana ila juhudi zinaendelea kufanyika ili kuboresha vifaa na miundombinu.
Baadhi ya wahitimu Zephania Ayola na Wakuru Kibina waliwaasa vijana wenzao wanaomaliza darasa la saba, kidato cha 4 au cha 6 kujiunga na Vyuo vya Veta ili waweze kupata ujuzi na kuwa mahiri katika fani za ufundi ili taifa liweze kupata mafundi na wataalamu wenye ujuzi halisi.
Ayola mwenye elimu ya kidato cha 6 ambaye alikuwa anasomea ufundi umeme wa majumbani alishauri serikali kuona umuhimu wa kuwapa mikopo wahitimu wa vyuo hivyo ili waweze kujiajiri kwa urahisi mara tu wanapohitimu.
Aidha aliomba serikali kutatua changamoto zinazokikabiri chuo hicho ikiwemo vifaa vya kujifunzia kwa vitendo, vitabu vya kujisomea katika maktaba na upungufu wa walimu.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba