December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi akisema jambo kwa timu ya uongozi wa afya ya Mkoa wa Mwanza kwenye kikao kazi cha kujadili vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga kilichofanyika Wilaya ya Misungwi.

“Vifo vya mama wajawazito havivumiliki tena ” – Mganga Mkuu wa Serikali

Na Mwandishi wetu,TimesMajira,Online,Mwanza

MGANGA Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi amesema kuwa Serikali haitovumia tena vifo vya akina mama wajawazito vinavyosababishwa na uzembe wa watumishi kazini.

Prof. Makubi ametoa kauli hiyo jana alipokuwa akifunga kikao kazi cha timu ya uongozi wa afya ya Mkoa wa Mwanza kilichofanyika Wilayani Misungwi kujadili vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga.

“Vifo vya akina mama wajawazito havivumiliki tena kwa sasa hivi kwenye hii dunia ambapo tumeingia uchumi wa kati ni lazima tutafute mbinu mpya na nzuri tuweze kuziendeleza na kuhakikisha kwamba ambaye amekuja kuleta maisha asifariki” amesema Prof. Makubi

Amesema siyo vifo vya akina mama wajawazito tu ndio vizuiwe bali hata vya watoto wachanga wanaozaliwa pia vidhibitiwe kwa wataalam wa afya kuhakikisha watoto hao wanazaliwa salama.

Prof. Makubi amesema Serikali imewekeza rasilimali nyingi kwenye sekta ya afya hivyo ni vyema matunda ya uwekezaji huo yakaenda kuonekana kupitia uboreshwaji wa huduma bora za afya ikiwemo kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga.

Amesema anashangazwa na vifo vingi vya akina mama wajawazito kutokea katika vituo vya kutolea huduma za afya na sio kwenye Jamii na kuwataka watumishi hao kujitafakari ni sehemu gani kuna changamoto ili zifanyiwe kazi na kudhibiti vifo hivyo.

“Nimefurahishwa kuona mmekutana hapa kutafakari, kwa hiyo mmeshaliona tatizo hamkusubiri Wizara ya Afya kuja kuwaambia mfanye nini, hilo ndio linanipa moyo mmejitambua na mmeamua kuchukua hatua wenyewe” amepongeza Prof. Makubi wa timu ya uongozi wa afya ya Mkoa wa Mwanza kwa kuanza kuchukua hatua.

Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Tiba anayesimamia Hospitali za Rufaa za Mikoa Dkt. Caroline Damian (kulia) pamoja na Katibu wa Mganga Mkuu wa Serikali Bi. Maurine Kunambi (kushoto) wakiwa kwenye kikao kazi cha kujadili vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga Mkoa wa Mwanza

Aidha,Prof. Makubi ametoa wito kwa Mikoa mingine iendeleze kile ambacho mkoa wa Mwanza imeanza kufanya kwa kufanya vikao vya tathimini na kuweka mikakati ya kudhibiti vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dkt. Thomas Rutachuzibwa amesema kuwa wameyapokea maelekezo yote aliyoyatoa Mganga Mkuu wa Serikali na watayafanyia kazi kuhakikisha vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga vinadhibitiwa mkoani humo.

“Ninakuahidi ndani ya miezi mitatu tutaanza kupata mabadiliko, tutakaa kwa muda uliobaki kuweka mpango kazi kuhakikisha tunaenda kutekeleza yale yote tuliyopanga ili kupunguza vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga” amesema Dkt. Rutachuzibwa

Dkt. Rutachuzibwa amesisitiza suala la wajibikaji kwa watumishi wa afya wakiwa kwenye maeneo yao ya kazi kwa kutambua wana wajibu upi na kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wananchi na kupunguza changamoto zilizopo maeneo yao ya kazi.