January 9, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

VETA:Taaluma ya ufundi stadi imeendelea kukua

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online,Dar

MWENYEKITI wa Bodi ya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Dkt.Peter Maduki amesema taaluma ya Ufundi Stadi imeendelea kukua na kusaidia kutatua changamoto mbalimbali katika jamii.

Dkt.Maduki ameyasema hayo katika Maonyesho ya 45 ya Biashara ya Kimatafa DITF yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam amesema VETA imekuwa ikibuni teknolojia na ubunifu mbalimbali pamoja na kufanya tafiti dhidi ya changamoto zinazoizunguka jamii.

Dkt.Maduki amesema,maonesho ya 45 ya mwaka huu wamejipanga kuonesha bunifu mbalimbali ikiwemo,maabara inayotembea ambayo itaondoa changamoto kubwa katika shule ambazo hazina maabara .

“Tumejipanga kuongeza uchumi katika sekta ya viwanda hasa kwa vijana wanaonza vyuo na hata waliopo kazini tayari” amesema Dkt.Maduki.

MWENYEKITI wa Bodi ya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Dkt Peter Maduki(mwenye suti nyeusi)alipotembelea katika Maonyesho ya 45 ya Biashara ya Kimatafa DITF 

Aidha ametoa wito kwa wafanyakazi waliopo kazini kwa muda mrefu kufika VETA kwa ajili ya kupata mafunzo mbalimbali ili kuongeza tija katika kazi zao.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa VETA Dk.Pancras Bujulu amesema katika maonesho ya mwaka huu wamejipanga kuonesha bidhaa za mikakati ikiwemo,vifaa vya kilimo,viwanda na ufugaji.

Amesema hivi sasa VETA imejiimarisha zaidi katika utoaji wa elimu kwa kuongeza vyuo 33 katika mikoa mbalimbali nchini na kufanya kuwa na jumla ya vyuo 71.

“Tanzania ni moja ya nchi inayoendelea katika mapinduzi ya viwanda hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kuanzisha vyuo vya Sayansi na Teknolojia ili wanafunzi wajue zaidi masuala ya ubunifu ambayo yanakwenda sambasamba na uchumi wa viwanda,”amesema Dk.Bujulu.

Dk.Bujulu amesema bunifu zao zinaongeza ufanisi zaidi katika jitihada za uchumi.