November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

VETA:Ipo haja vyeti vya mafunzo ya JKT kutambuliwa

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Mbeya

MENEJA  Uhusiano wa Mamlaka ya Ufundi Stadi VETA Sitta Peter kuna manufaa makubwa kwa vijana wa Jeshi la Kujenga Taifa wanaohitimu mafunzo ya kujitolea katika Jeshi hilo kutunukiwa vyeti ambavyo vinatambulika na VETA ili kuwawezesha kuendelea na elimu ya juu zaidi ya ufundi.

Sitta ametoa kauli hiyo mkoani Mbeya kufuatia ziara ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa  katika Banda la Mamlaka hiyo kwenye maonyesho ya Nane Nane yanayofanyika Kitaifa viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.

Akiwa katika banda hilo Waziri Bashungwa alizungumzia kuhusu kuingiwa kwa makubaliano baina ya Wizara yake kupitia JKT kutokana na mafunzo ya ufundi ambayo vijana wa kujitolea wamekuwa wakipatiwa wawapo makambini.

“Waziri Bashungwa amezungumzia mawazo mbalimbali na ametoa ushauri na maelekezo ambayo nasi tunaona  manufaa makubwa kama makubaliano hayo yataingiwa ,kwa maana kwamba vijana wanaweza wakatumia muda wao wa mafunzo kujifunza ukakamavu na uzalendo kwa miezi kadhaa ,na miezi mingine wakajifunza ufundi stadi katika maeneo mbalimbali na wakatunikiwa vyeti, ama zile programu za mafunzo zikawa ‘acredited’  kiasi kwamba baada ya mafunzo wakapata vyeti,

“Kwa hiyo hata kijana  anapomaliza mafunzo ya JKT akirudi mtaani asiwe mtu ambaye anabaki hana kitu cha kufanya bali awe na ujuzi ambao utautumia kujiajiri na kukuza uchumi wake lakini kuchangia pato la Taifa.”amesema Sitta na kuongeza kuwa

“Hii itawasaidia sana vijana ,kwa sababu wengi wao wakishajifunza huko kwa sababu ya kukosa cheti kinachotambua hayo mafunzo unakuta hata fursa za kuendeleza huo ujuzi wao unakuwa ni changamoto lakini pia wengi wanaamua kusubiri zipatikane kazi angalau hata za kwenye makampuni ya ulinzi.”