November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

VETA waja na maabara inayotembea

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Chang’ombe imetegeneza maabara inayotembea itakuwa ikitoa mafunzo ya vitendo kwa masomo ya sayansi na Fizikia kwa shule za msingi na sekondari.

Akizungumza katika Maonyesho ya 45 ya Kimataifa ya biashara ya Dar es Salaam (DITF) yaliyoanza Juni 28 mwaka huu, Mwalimu kutoka VETA Chang’ombe, Emmanuel Bakula amesema, tayari maabara hiyo itatumika imeshapewa kibali na itatumika katika shule ambazo zinauhaba wa maabara .

Amesema kuwa, maabara hiyo imetengenezwa 2020 na mwaka huu iliweza kupelekwa katika maonyesho ya mashindano ya Kisayansi, Teknolojia na Ubunifu(MAKISATU) na kufanikiwa kushinda nafasi ya kwanza.

“Kwa sasa ipo tayari kwa matumizi na inaweza kwenda mahali popote itakapohitajika hasa kwa shule ambazo zina uhitaji na siziso na maabara au zenye maabara lakini hazina vifaa,” amesema Bakula.

Mmoja wa wanafunzi walioshiriki kubuni kubuni maabara hiyo, Hawa Kindamba ameweka wazi kuwa, ubunifu wa Maabara hiyo utasaidia kutafuta changamoto ya baadhi ya wanafunzi kutopenda masomo ya sayansi kutokana ukosefu wa maabara.

Lakini pia amewataka wanafunzi wa kike kupenda masomo ya sayansi kwa kuwa hayana ugumu wowote kama wengi wanavyodhani kutokana na imani waliyojijengea.