December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

VETA Kihonda,yawakaribisha wawekezaji kuwekeza sekta ya kilimo

Na Penina Malundo,timesmajira, Online

MAMLAKA  ya  Elimu na Ufundi Stadi (VETA) ,Kihonda Morogoro,kimewasihi wawekezaji nchini  kuja kuwekeza katika sekta ya kilimo kwani upatikanaji wa malighafi za kilimo kwa sasa zimekuwa zikipatikana kwa urahisi ukilinganisha na miaka ya nyuma.

Akizungumza leo jijinj Dar es Salaam,Mkufunzi wa  Chuo cha Veta,Kihonda Mhandisi Joseph Kimako amesema urahisi wa upatikanaji wa malighafi za kilimo unakuja baada ya vyuo vya VETA nchini kufundisha programu mbalimbali ikiwemo ya masuala ya Ufundi wa dhana  ya Mitambo ya Kilimo.

Amesema kwa Chuo cha ufundi VETA,Kihonda  kimekuwa kikifundisha namna ya uandaaji wa udongo ambapo unamrahisishia mkulima katika kilimo chake kulima mazao mengi bila kupoteza mbegu wakati wa kuotesha mazao hayo.

“Kauli mbiu ya mwaka huu katika maonesho haya yanasema Tanzania ni mahali sahihi kwa uwekezaji na biashara hivyo teknolojia hii ya udongo ambao unatokana na mvuke ni rahisi inayomuwezesha mkulima kuweza kupanda miche na kuandaa udongo kwa urahisi zaidi,”amesema 

Mhandisi Joseph Kimako akionyesha teknolojia ya Mvuke inavyotengeneza udongo kwa waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam.

Amesema  Chuo chao kimeamua kuja na udongo wa mvuke ambao ni rahisi zaidi kwa wakulima katika mazao yao na haupotezi mbegu nyingi chini.

“Udongo huu unatumia makapi  au mabaki  ya mpunga unachanganya na udongo wa msituni ambapo unawekwa katika mtambo wenye maji yanayochemka na kufikia nyuzi joto 100,ambapo udongo huo unawekwa katika mtambo huo na kukaa dakika 20 au 30 kwaajili ya kuua masalia ya wadudu pamoja na magugu”amesema

Amesema baada ya kuua masalia hayo ya wadudu udongo utolewa na kukaushwa kisha kuwa tayari kutumika na wakulima njia ya kuandaa ni rahisi na rafiki kwa wakulima.

Mhandisi Kimako ametaja baadhi ya faida katika kutumia udongo huo ni pamoja kumsaidia mkulima kupunguza upotevu wa mbegu wakati wa kupanda ,kujua idadi sahihi ya Miche mkulima anayotaka kupanda pamoja na udongo huu utumia mbegu chache kupanda.

“Unajua tumezoea kutumia njia ya kiasili kupanda mbegu njia hiyo inafanya kupoteza mbegu nyingi chini ,wadudu uzila mbegu hizo hivyo kufanya mkulima kupoteza mbegu,”amesema 

Aidha amesema udongo huo unamsaidia mkulima kupata njia rahisi ya kupanda mbegu za mazao yake kiurahisi zaidi kwani  haina elimu kubwa ya upandaji wa mbegu na kuota vizuri.