September 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

VAR kutumika Ligi Kuu Tanzania msimu ujao

*Ampongeza Rais Samia, atoa msamaha uingizwaji VAR

Na Mwandishi Wetu, Timesmajiraonline, Dodoma

WAZIRI wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania, zitaanza kutumika teknolojia ya video za kumsaidia mwamuizi (VAR), ili kuhakikisha matokeo yanayopatikana uwanjani kwa haki.

Dkt. Mwigulu Nchemba pia alipendekeza kutoa msamaha kwenye uingizaji wa mashine za ‘’VAR’’ na vifaa vyake kwa ufafanuzi utakaotolewa hapo baadaye huku akisema uamuzi huo utasaidia kuwa na ‘’VAR’’ za kutosha katika viwanja vyote Tanzania.

Akiwasilisha Bajeti Kuu ya Serikali ya Mwaka wa Fedha 2024/2025 Bungeni Jijini Dodoma Juni 13, mwaka huu Waziri Mwigulu, alisema serikali ilishatunga sheria inayotoa msamaha kwenye uingizaji wa nyasi bandia na vifaa vyake ili eneo la kuchezea, yaani pitch kwenye viwanja mbalimbali ziwe kwenye ubora.

“Msimu ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania tutaanza kutumia ‘’VAR’’ ili kuhakikisha matokeo yanayopatikana uwanjani yanakuwa ya haki maana kuna timu zimezidi msimu mmoja penati 10, halafu zikifungwa zenyewe magoli yanakataliwa.

“Na ili tuwe na ‘VAR’ za kutosha katika viwanja vyote, naleta pendekezo la kutoa msamaha kwenye uingizaji wa mashine za ”VAR” na vifaa vyake kwa ufafanuzi utakaotolewa hapo baadae,” alisema Dkt. Migulu.

Hata hivyo alisema, Serikali ya Awamu ya Sita inatambua umuhimu wa michezo, sanaa na burudani katika kukuza ajira hususani kwa vijana. Kwa kuzingatia hilo, Serikali imeendelea kuwaunganisha wasanii wa Tanzania na soko la kimataifa kupitia mikutano na matamasha mbalimbali kuhakikisha kazi za ubunifu wao zinalindwa.

Aidha, alisema kwa upande wa michezo, Serikali imeendelea kujenga misingi ya uibuaji na uendelezaji wa vipaji kuanzia mashuleni ambayo imesaidia kuongeza ajira na kipato kwa wachezaji wanaosajiliwa katika timu mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Alisema, kufuatia hatua hiyo ya uendelezaji wa vipaji, imewezesha timu ya taifa ya mpira wa miguu Taifa Stars kushiriki mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) kwa mara ya tatu katika historia ya Taifa letu na Timu ya Taifa ya wanawake ya mpira wa miguu Twiga Stars kufuzu kucheza mashindano ya WAFCON ambayo yatafanyika mwaka 2024 nchini Morocco.

Katika hatua nyingine Dkt. Mwigulu Nchemba alisema kufuatia jitihada za makusudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha sekta ya michezo nchini, Tanzania itakuwa mwenyeji wa michuano ya kombe la AFCON ya mwaka 2027 kwa kushirikiana na nchi za Uganda na Kenya.

“Nipende kuwahakikishia kuwa, Serikali imejipanga vyema juu ya maandalizi ya michuano hiyo ikiwemo ujenzi wa uwanja wa mpira wa Samia jijini Arusha kama alivyowasilisha Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo.

“Nitoe rai kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania kuanza maandalizi ya timu yetu ya Taifa mapema ili hatimaye tulibakize kombe hilo hapa nyumbani,” alisema Dkt Nchemba.

Katika hatua nyingine Dkt. Mwigulu Nchemba alisema Serikali imejiandaa kujenga viwanja vipya na kukarabati baadhi ya viwanja vilivyopo kwenye eneo la kuchezea, yaani pitch kwenye viwanja mbalimbali.

Hata hivyo aliipongeza timu ya Azam FC kwa kushika nafasi ya pili katika mashindano ya Ligi kuu ya NBC na kufuzu kushiriki mashindano ya Klabu Bingwa ya Afrika. Lakini pia aliipongeza timu ya Coastal Union kwa kufuzu kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya muda mrefu.

“Kwenye mafanikio ya timu ya Coastal Union, nimpongeze kwa dhati Waziri wa Afya Ummy Mwalimu, Mbunge wa Tanga Mjini, kwa kujitoa kwa hali na mali ikiwa ni pamoja na kuhudhuria katika uwanja wa Mkwakwani na viwanja vingine bila kukosa na kushirikiana na wadau wengine kuiwezesha timu hiyo kufuzu kushiriki mashindano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika,” alisema.

Pia, alimpongeza GSM kwa uwekezaji mzuri alioufanya ambao umebadilisha kabisa taswira na uwezo wa kiuchezaji wa timu ya Yanga. Mafanikio hayo yalitokana na uwekezaji mzuri uliofanywa na muwekezaji huyo.

“Napenda nitoe pongezi kwa Menejimenti Bora ya timu chini ya Eng. Hersi Saidi kwa kuiongoza vyema timu ya wananchi Yanga na kuipeperusha bendera ya nchi yetu katika medani za kimataifa.

“Kama tunavyofahamu, Tanzania iliingiza timu mbili katika hatua ya robo fainali ya Klabu Bingwa Afrika, ikiwa ni kwa mara ya kwanza katika historia ya soka nchini.

“Pamoja na kwamba wenzetu Simba walipigwa ndani nje katika hatua hiyo lakini ni sehemu ya kujifunza na kujipanga upya. Kipekee, niipongeze timu ya Yanga kwa kuitoa jasho timu ya Mamelodi Sundowns.

“Nina hakika siku ile ya mechi ya mwisho kule Afrika Kusini, wale wachezaji wa Mamelodi Sundowns walilala na viatu kufuatia kitu kizito walichokumbana nacho uwanjani.” alisema Mwigulu Mchemba.

Aidha, alisema mafanikio hayo yalichangiwa kwa kiasi kikubwa na hamasa ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alikuwa akitoa shilingi milioni tano kwa kila goli linalofungwa katika hatua ya makundi na shilingi milioni kumi kuanzia hatua ya robo fainali.

“Hivyo, kwa namna ya pekee naomba nitoe pongezi kwa Rais wetu kwa ubunifu huo ambao umeliletea Taifa letu sifa na heshima kubwa katika nyanja ya michezo.

“Rai yangu kuwa tuendelee kuhamasisha michezo mingine ili nchi yetu iweze kushiriki katika mashindano mbalimbali ya kimataifa na hatimaye kurudi na tuzo au makombe,” alisema