June 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

UWT yalaani tukio la mauaji ya mtoto mwenye Ualbino

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) imelaani na kukemea vikali matukio ya kikatili na ya kinyama dhidi ya watu wenye ulemavu na kuiomba serikali kupitia vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha wahusika wanatafutwa, wanakamatwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.

Hii ni baada ya kutokea kwa mauaji ya mtoto mwenye umri wa miaka miwili aitwaye Asimwe Novarti aliyeibiwa na watu wasiojulikana mnamo tarehe 30 Mei, 2024 na kukutwa akiwa amekufa tarehe 17 Juni 2024 huku mwili wake ukiwa umekatwa katwa na kutolewa baadhi ya viungo kwenye mwili wake katika Kitongoji cha Mbale, Kijiji cha Bulamula, Kata ya Kamachumu, Wilaya ya Muleba, Mkoa wa Kagera.

Ombi hilo limetolewa na Katibu Mkuu wa UWT Taifa, Suzan Kunambi leo Jijini Dar es Salaam na kusema kuwa matukio hayo ya kikatili yanavunja haki, utu, na heshima ya kibinadamu kama ilivyoainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Sheria za Nchi pamoja na Mikatataba ya Kimataifa ya Haki za Binadamu.

Kunambi ameitaka kuwa na hofu ya Mungu na kuachana na vitendo vya Imani za kishirikina

“Jamii iwe na hofu ya Mwenyezi Mungu na kuachana na vitendo vya Imani za kishirikina zinazopelekea kutoa uhai kwa watu wasio na hatia.”

Aidha ameiomba Jamii kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa za watu wote wanaojihusisha na vitendo hivyo ili vyombo vya ulinzi vichukue hatua stahiki.

Pia amesema ni vyema ulinzi shirikishi uendelee kwa viongozi ngazi zote kuanzia Kitongoji, Kijiji, Mtaa, Kata, Wilaya na Mikoa ili kuwalinda watu wenye ulemavu.

“Wenye Ulemavu ni ndugu zetu, wanahaki ya kufurahia maisha yao kama wengine katika jamii” Amesisitiza