Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma
MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi Tanzania (UWT)Mary Chatanda amelaani tukio la shambulio la kudhuru mwili alilofanyiwa Mwenezi wa Baraza la Wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),BAWACHA Sigilada Mligo lililotokea Machi 25,2025 Mkoani Njombe.
Amesema kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe Machi 26,2025 kuhusu tukio hilo alieleza kuwa Sigilada Mligo ameshambuliwa na mmoja wa walinzi wa Chama hicho anayefahamika kwa jina la Noel Olivale baada ya kutokea mzozo ndani ya kikao cha ndani cha chama hicho.
Chatanda amesema hayo jijini hapa leo Machi 28,2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kulaani tukio hilo.
“Kwakuwa UWT moja ya madhumini na majukumu ya UWT pamoja na mengine kwa mujibu wa kifungu (f)chombo cha ukombozi wa wanawake wa Tanzania dhidi ya unyanyasaji,ukandamizaji,uonevu na mila zote zinazorudisha nyuma maendeleo ya wanawake.
“Hivyo shambulio la kudhuru mwili dhidi ya Mwanamke wa Tanzania ndugu Sigilada Muligo Mwenezi wa BAWACHA lililopelekea maumivu hadi kufikia hatua kulazwa ni unyanyasaji, ukandamizaji na uonevu dhidi ya mwanamke jambo ambalo ni baya sana na UWT tunalipinga kwa nguvu kubwa na kukemea,”amesema Chatanda.
Chatanda amesema UWT inasikitishwa kwakuwa tukio hilo limetokea kwenye mazingira ambayo alikuwepo kiongozi wa ngazi za juu Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA ndugu John Heche ambapo inasemekana hakuchukua hatua yoyote na mpaka sasa hakuna tamko lolote kutoka kwake kama kiongozi ambaye alikuwa Mwenyekiti wa kikao cha ndani kilichotokea mzozo.
“Hatua ya kukaa kimya kwa Makamu Mwenyekiti ndugu Heche na uongozi wa juu wa chama hicho ni kiashiria tosha kuwa chama hicho kina mfumo dume hakiwathamini wanawake na kwamba iwe ishara kwa viongozi wanawake wa chama hicho,”amesema Chatanda.
Kutokana na hayo Chatanda amelitaka Jeshi la Polisi kuendelea kumsaka mtuhumiwa na kumfikisha katika vyombo vya sheria kwakuwa wapo tayari kutoa msaada wa kisheria kwa kutoa mwanasheria ili haki iweze kupatikana kwa mhanga wa tukio hilo.
“Tunatoa wito kwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Njombe kuendelea kumsaka mtuhumiwa na kumfikisha kwenye vyombo vya sheria,UWT ipo tayari kumuwekea mwanasheria ili haki iweze kupatikana,”amesema Chatanda
Vilevile ameiomba Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa kufuatilia kwa karibu uanzishwaji wa madawati ya jinsia kwa vyama vya siasa na kuangalia utekelezaji wa majukumu yake ili madawati hayo yawe na uwezo na mamlaka ya kuchukua hatua dhidi ya vitendo vya unyanyasaji na ukandamizaji dhidi ya wanawake kwakuwa sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 2023 imevitaka vyama vya siasa kuanzisha madawati hayo.
Pamoja na hayo chatanda amewahamasisha wanawake kujiandaa na kujitokeza muda ukifika wa kuchukua fomu za nafasi ya ubunge wa majimbo na udiwani wa kata ndani ya vyama mbali mbali kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu 2025.
More Stories
Mo Dewji na Urithi anaoujenga ,unavyoenda mbali zaidi ya mafanikio binafsi
Mulika Community kusaidia Serikali kukomesha vitendo vya ukatili
TMDA yashinda tuzo za PRST ya Umahiri katika kampeni bora ya utoaji elimu jamii