Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
JUMUIYA ya Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoani Tabora (UWT) wamesherehekea miaka 46 ya kuzaliwa kwa chama hicho kwa kutembelea miradi ya maendeleo ikiwemo ya uzalishaji mali, kuendesha harambee ya kuboresha miradi yao na kutoa msaada kwa watoto wa shule na akinamama.
Akitoa taarifa ya Jumuiya hiyo mbele ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa, Hassan Wakasuvi, Katibu wa UWT Mkoani hapa Rhoda Madaha alisema wanaungana na wanaCCM wote kumpongeza Mwenyekiti wa Taifa wa chama na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayofanya.
Alisema UWT Tabora wataendelea kuunga mkono juhudi zote zinazofanywa na Rais Samia na kutekeleza maagizo yake kwa kila Jumuiya kuwa na miradi endelevu ya kiuchumi.
Alisema wanajivunia kuwa na Rais mwenye maono makubwa ya maendeleo na anayesimamia kwa dhati utekelezaji ilani ya uchaguzi ya chama ili kuwaletea maendeleo ya kweli wananchi wake kupitia ilani ya uchaguzi. Madaha alisisitiza kuwa wanawake wote wa Mkoa huo wamehamasishwa kuanzisha miradi ya uzalishaji mali katika sekta ya kilimo ili kujikwamua kiuchumi ambapo zaidi ya ekari 1,056 za alizeti zimelimwa na kupandwa.
‘Hadi sasa wana UWT wa kata 202 kati ya kata 206 za Mkoa mzima wameanzisha miradi yao ya kilimo cha alizeti, kata 4 tu ndio bado, nazo zinajipanga kwa ajili ya kuanzisha mradi wao’, alisema.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa aliwapongeza Viongozi wa UWT kwa kusimamia vyema Jumuiya hiyo na kuhamasisha wanachama wao kuanzisha miradi ya kilimo cha alizeti, mahindi, mpunga, viazi na mengineyo ili kuwaingizia kipato.
Aidha alipongeza maono yao mazuri ya kuunganisha wanachama wao ili kufanikisha mipango yao ikiwemo ubunifu mkubwa ambao umewezesha harambee kuwaingizia zaidi ya sh mil 6 kwa ajili ya kuboresha mradi wao wa shule ya awali.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutoka Mkoani hapa Mohamed Nassoro Hamdan (Meddy) aliwataka Viongozi wa Jumuiya zote kubuni miradi inayotekelezeka na yenye tija itakayowaingizia mapato.
Naye Mwenyekiti wa UWT Mkoani hapa Bi.Mwanne Mchemba alisema wamejipanga vizuri ili kuhakikisha matawi yote ya UWT katika kila kata na wilaya yanakuwa na miradi endelevu ya kuwaingizia mapato.
More Stories
Walimu S/ Sekondari Ilala wafundwa juu ya maadili ya wanafunzi
Dkt. Samia afungua skuli ya sekondari Misufini, Bumbwini
Rais Mwinyi: Barabara Pemba zitajengwa kwa lami