October 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

UWT Songwe yaonya makada wanaoshushiana hadhi mitandaoni

Na Moses Ng’wat, Songwe,Timesmajira

UMOJA wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Mkoa wa Songwe umekemea baadhi ya wanachama wake kuacha tabia ya kutumia vibaya mitandao ya kijamii kwa kuendesha majibizano, kuzodoana na kushushiana hadhi.

Badala yake, umewataka wanawake wa jumuiya hiyo kuendelea kuwa wamoja ili kukiletea ushindi chama hicho kwenye chaguzi zijazo za serikali za mitaa na uchaguzi Mkuu wa hapo mwakani 2025.

Karipio hilo limetolewa leo Agosti 29, 2024 na Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Songwe, Mwl. Emelia Mwakyoma, wakati akizungumza na waandishi wa habari ikiwa ni siku moja baada ya jumuiya hiyo kufanya kikao cha kamati ya utekeleza, ikiwemo kujadili masuala ya nidhamu.

Amesema pamoja na wajumbe wa kikao hicho kupongeza viongozi mnalimbali wa serikali na chama, pia walijadili suala la nidhamu kwa lengo la kuijenga jumuiya na chama hasa katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye chaguzi hasa baada ya kujitokeza tabia ya baadhi ya wanawake kutumia mitandao ya kijamii kuibua majibizano, kuzodoana ikiwemo kushushiana hadhi, jambo ambalo si utaratibu wa chama.

“Naomba nitumie fursa hii kuwasihi wanawake wenzangu wanaotumia vibaya magrupu ya yaliyoanzishwa kwenye jumuiya zetu kupitia mitandao ya kijamii tuache majibizano, kuambiana mambo tofauti, kuzodoana, ikiwemo kushushiana hadhi kwani kila mtuu anafaa kwenye nafasi aliyonayo na wote tunahitaji kwa ajili ya kukijenga chama hasa kwenye mkoa wetu wa Songwe” amesema Mwl. Mwakyoma.

Amesema viongozi wa jumuiya hiyo na chama mkoa wa Songwe kwa sasa uko imara sana hivyo wale wote watakaoendelea kukiuka taratibu na miongozo ya chama, ikiwemo kutumia vibaya mitandao ya kijamii watachukuliwa hatua kali ikiwemo kufikishwa kwenye vikao vya juu vya maamuzi.

Aidha, UWT Mkoa wa Songwe umempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan, kwa kuwekeza miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo sekta ya afya na kufanya mapinduzi makunwa ya matibabu kwa kuleta vifaa vya kisasa hali ambayo imeondoa usumbufu kwa wananchi kwenda nje ya nchi kufuata matibabu.

“Tunampongeza sana Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan na Mwenyekiti wetu wa chama Taifa kwani katika uongozi wake ameendelea kufanya mambo makubwa ikiwemo utekelezaji wa miradi mikubwa ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa iSGR ‘ amesema Mwl. Mwakyoma.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti huyo wa UWT mkoa wa Songwe, amesema kuwa mapema mwezi ujao wa Septemba, 2024 jumuiya hiyo inatarajia kuanza ziara za kuhamasisha wanawake kujitokeza na kushiriki kwenye chaguzi zijazo za serikali za mitaa na uchaguzi Mkuu.