Na Yusuph Mussa, TimesMajira Online, Korogwe
Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Mkoa wa Tanga, na Jumuiya ya Wazazi mkoani humo, wote wamepata uongozi mpya baada ya uchaguzi uliofanyika Novemba 17 na 18, 2022 wilayani Korogwe.
Kwa upande wa UWT, Msimamizi Mkuu wa Uchaguzi huo ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Muheza Halima Bulembo, alimtangaza Al- Shaymaa Kweygir kuwa Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Tanga.
Kweygir alipata kura 442 na kuwashinda wenzake wawili, Rahma Likate aliyepata kura 125, na Jokha Mjenga aliyeambulia kura 23.
Mwantumu Mahiza aliibuka mshindi wa nafasi ya Mjumbe wa Baraza Kuu UWT Taifa kwa kura 493, na kuwaacha mbali washindani wake Jane Gonsalves aliyepata kura 57, na Saada Emmanuel kura 26.
Na Rukia Mapinda alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Mkoa wa Tanga.
Msimamizi Mkuu wa Uchaguzi wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Tanga ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Tanga Hashim Mgandilwa alimtangaza Alhaji Hassan Mbezi kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Tanga kwa kupata kura 587, na kumshinda Mwenyekiti anaemaliza muda wake Sadick Shedaffa ‘Jeingata’ aliyepata kura 226.
Hassan Bomboka alitwaa nafasi ya Mjumbe wa Baraza Kuu Jumuiya ya Wazazi Taifa kwa kupata kura 666, na kumshinda Benadetha Ngwilizi ‘Makihiyo’ aliyepata kura 216, huku Katibu wa Elimu, Malezi na Mazingira, akichaguliwa Salim Badi.
Akizungumza na mwandishi wa habari, mara baada ya uchaguzi huo, Mwenyekiti mpya Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Tanga, Mbezi, alisema yapo mambo atayafanyia kazi ili kuimarisha jumuiya hiyo ikiwemo kila wilaya kuwa na miradi ili kuondoa tabia ya ombaomba kunapotokea kuwa na shughuli za jumuiya.
Pia shule za sekondari zinazomilikiwa na jumuiya hiyo ikiwemo Mombo iliyopo Wilaya ya Korogwe, Kideleko ya Handeni, Boza ya Pangani, Kwemvumo ya Lushoto, na Mbaramo ya Muheza, ziwe na miradi yao ili kujitegemea.
“Nawashukuru Wajumbe kwa kunipa dhamana hii, lakini shukrani pekee nazipeleka kwa Mwenyekiti wa chama chetu na Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa kuniamini, na kurudisha jina langu. Nitafanya kazi kwa ushirikiano wa pamoja ili jumuiya yetu iwe imara.
“Tunataka shule ya Mombo na Boza kupanda mkonge, na ile ya Mbaramo kupanda michungwa. Hiyo itasaidia kuwa na miradi itakayoingiza kipato. Pia tunataka kila wilaya kuwa na miradi yake ili kuondoa tabia ya ombaomba kwenye jumuiya” alisema Mbezi.
More Stories
AZAKI yawasilisha mapendekezo yao kwa Serikali katika kuboresha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050
CP.Wakilyamba :Uvamizi maeneo ya hifadhi ya taifa katavi haukubaliki
Watu wawili wanaodhaniwa majambazi wapigwa risasi na Polisi