January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

UWT Katavi yaitaka jamii kushughulikia kiini vitendo vya ukatili wa kijinsia

Na George Mwigulu,Timesmajiraonline, Katavi.

UMOJA wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi, (UWT)Mkoa wa Katavi umeitaka jamii kusimamia vema maadili na malezi ya watoto ili kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia nchini.

Mwenyekiti wa umoja huo, Fortunata Kabeja hivi karibuni amezungumza na waandishi wa habari na kufichua mmomonyoko wa maadili unachangiwa na baadhi ya wazazi na walezi kushindwa kuwajibika kimalezi.

Mbali ya kuwanyoshea kidole wazazi na walezi, Kiongozi huyo ametoa wito kwao kushikamana kwenye malezi ya familia kwani familia ni chimbuko la jamii ya sasa na ijayo.

“Jamii inawajibu wa kutoa malezi yanayozingatia utamaduni wa Kitanzania, utakuwa mwanzo wa kupiga hatua ya kujenga maadili na kukomesha ukatili ambao umeripotiwa katika baadhi ya maeneo kuwa ni chanzo cha ulemavu wa kudumu kwa watu” Amesema Kabeja

Aidha ameongeza kuwa Mkoa wa Katavi bila ukatili wa kijisia unawezekana pale ambapo ongezeko la harakati dhidi ya makundi yanayotetea haki pamoja na yake yanayosimamia masuala ya wanawake na hivyo yataimarisha zaidi mabadiliko ya sheria ambazo zitachochea utetezi wa haki za wanawake, halikadhalika kuimarisha mustakabali wa watetezi wa haki za binadamu.

Hatua ya Umoja huo zilizochukuliwa ni kujitokeza hadharani kupitia kongamano la wanawake la kupinga ukatili wa kijinsia na kutoa jumbe mbalimbali ambazo ni pamoja na wanawake wapewe nafasi wanayo haki ya kugombea na kuchaguliwa serikali za mitaa 2024 na uchaguzi mkuu 2025.

Ujumbe mwingine ni “wanawake tujitokeze kwa wingi kwenda kugombea nafasi mbalimbali za uongozi tunaweza na jisajiri katika mfumo wa Tehama ili uwe na sifa ya kuwa mwananchama wa UWT”.

Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Katavi, Kiame John ameweka wazi kuwa kwa mwaka 2023 matukio 3144 ya ukatili yameripotiwa na wanawake pekee huku matukio 758 kwa wanaume.

“Tumebaini  vitendo vya ukatili wa kijisia vimepelekea ulemavu ambapo kwa mwaka 2023 ni watu 35 kupitia ukatili wamepata ulemavu wa kudumu” Amesema John.

Ni wazi vitendo vya ukatili wa kijisia kwa tafiti zilizofanywa mwaka 2015/16 (Chazo cha tafiti hakijawekwa wazi na John) Mkoa wa Katavi ulikuwa unaongoza kwa asilimia 45 kuwa na mimba nyingi za utotoni.

Kwa utafiti wa mwaka 2022 imebainishwa mkoa huo kwa sasa tatizo hilo ni asilimia 34 pungufu kwa asilimia 10 ikilinganishwa na hapo awali ambapo kwa mkoa wa Songwe ukiwa unaongoza kwa asilimia 45 nchini.

Ameongeza “ Takwimu za mwaka 2023 watoto wenye umri kati ya miaka 10 hadi 14 kulikuwa na watoto 60  wajawazito kwa upande wa umri wa miaka 15 hadi 19 kulikuwa na watoto 13,409 wajawazito”.

Katibu wa UWT Mkoa wa Katavi, Edina Buzima amesema juhudi kubwa ya kudhibiti vitendo vya ukatili wa kijisia wanazofanya ni kupaza sauti kwa jamii ili kwa pamoja kuweza kupinga ukatili huo.

“Hatuwezi kukubali kama jamii kuona ukatili wa kijisia. Tumejiimarisha kwa kupaza sauti zinatoa elimu juu athari mbaya kwa ustawi wa taifa letu zinazoweza kujitokeza kupitia ukatili wa kijisia…athari mbaya kwenye jamii tumeziona ni pamoja na watu wenye ulemavu wa ngozi kutolewa uhai” Amsema Edina.

Amesema kuwa Kuimarisha vita dhidi ya ukatili wa kijisia kwa kushirikiana na makundi mengine ya harakati za kijamii na kisiasa ni nyezo muhimu ya kuzuia kurejeshwa nyuma za haki za wanawake na watoto na hatimaye kutokomeza ukatili ufanikiwe.