December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

UWEZO FESTIVAL yafana Dar

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

Wazazi wametakiwa kubadilika na kuwaruhusu watoto wao kushiriki katika majukwaa ya kuonyesha vipaji vyao ili waweze kuwa na nyenzo nyingi za kupambana na ukosefu wa ajira.

Hayo yamesemwa jana Jijini Dar es Salaam na Mratibu wa Kitaifa wa miradi kutoka Shirika la Great Hope Foundation, Noele Mahuvi wakati wa tamasha la UWEZO FESTIVAL ambalo ni la wanafunzi kuonyesha uwezo wao, linalofanyika kila mwaka kwenye shule mbalimbali za sekondari kupitia miradi yao miwili ya uwezo Award na uwezo Bonanza.

“Uwezo Bonanza tunawahimiza watoto watimize vipaji vyao, wavitambue, wavithamini ili wanavyotoka shule kwenye soko la ajira viweze kuwasaidia kupata ajira au wajiajiri”

“Miradi ya uwezo award imelenga kwamba wanafunzi ujuzi wa kijasiliamali, kwamba wajifunze kuwa wajasiriamali wakiwa shuleni wakitoka wapate nafasi ya kuweza kujiajiri au kuajirika kwa urahisi”

Mahuvi amesema katika tamasha hilo, shule 25 zimepewa tuzo mbalimbali kwa upande wa wanafunzi wenye vipaji vya kuimba, kucheza, wanamitindo n.k

“uwezo Award wanatoa tuzo kwa shule 25 , tuzo 3 ngazi ya dhahabu, tuzo 12 ngazi ya silver na tuzo 10 ngazi ya shaba”

Kuhusu matokeo ya mradi, amesema mradi umekua,  wanafunzi wamekua wengi na uhitaji umekua mkubwa kwasababu walikua wakiyakosa majukwaa kama hayo kutoa kile walichonacho.

“Miradi ya uwezo mashuleni ilianza mwaka 2016 na huu ni mwaka wa 8, tulianza na shule 20 na sasa tumefikia shule 250 kwa mwaka na kwa mwaka huu tumefikia shule 258 kwenye miradi yote miwili” Amesema.

Kwa upande wake Mwanafunzi kutoka shule ya Sekondari Juhudi, Imani Mpali amesema jukwaa hilo linawasaidia kujiamini wanapokua sehemu mbalimbali lakini pia kuwaza mbali zaidi katika kubuni mradi wa kujikwamua kiuchumi.

“Katika miradi ya uwezo tunatengeneza sabauni na vitu vingine kwani ni chachu ya sisi hata tukitoka shule unaweza ukajiongeza kufanya vitu mbalimbali ukajiongezea kipato”

“Uwezo Festival inatufanya kuweza kujuana na watu mbalimbali wa shule nyingine ambapo tunaweza kushirikiana na kupeana maarifa ambayo hatukuwa tunayajua”

Ameitaka serikali kuyaunga mkono Mashirika kama hayo ili fursa ziweze kuendelea kuwepo ili ziwafikiw wanafunzi mashuleni.

Naye Mwanafunzi kutoka shule ya Sekondari Kichanga Sekondari, Amina Majaliwa amewataka wazazi wawape ushirikiano watoto wao wenye vipaji ili waweze kufanya vitu wanavyovitaka kuviishi katika maisha yao.

Matukio mbalimbali katika picha