December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Uwekezaji DIT kuzalisha wataalamu wa teknolojia

Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online DSM

KATIBU Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo amesema Serikali inafanya uwekezaji mkubwa kwenye Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) ili kuhakikisha inatoa wataalamu wengi katika eneo la Teknolojia.

Prof. Nombo amesema hayo jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake katika taasisi hiyo iliyokuwa na lengo la kujionea shughuli zinazoendelea kutekelezwa na kuwapa mwelekeo wa Serikali ambao ni kutoa elimu bora ya Amali na kuimarisha ukuzaji na matumizi Teknolojia.

Amesema katika nchi yetu DIT ni Taasisi inayotoa wataalamu katika eneo la Teknolojia na Uhandisi na kwamba ina vifaa vingi vya kufundishia na kujifunzia na kuwapa changamoto ya kufanya vizuri ili Taasisi hiyo iwe kama taasisi ya MIT ya Marekani.

“Taasisi hii ina vifaa ambavyo vinawezesha kuwa na teknolojia mbalimbali ambazo zitatatua changamoto mbalimbali katika nchi yetu, lakini pia nimeona kuna Kampuni Tanzu ya DIT hakikisheni mnaiimarisha kampuni hiyo iweze kujitegemea na kukiiingizia Chuo kipato,”amesema Prof. Nombo.

Akizungumzia ujenzi unaoendelea Chuoni hapo Prof. Nombo amemtaka mkandarasi anaejenga Kituo hicho cha Umahiri wa TEHAMA cha Kikanda cha Afrika Mashariki (RAFIKI) na mabweni ya wanafunzi kuhakikisha anaongeza kasi ya ujenzi ili ukamilike kwa ubora na kwa wakati.

“Mmeniambia mabweni haya yapo asilimia 17 ya ujenzi, Kituo cha Umahiri wa TEHAMA cha Kikanda cha Afrika Mashariki (RAFIKI) kipo asilimia 15 na ujenzi wote kwa pamoja unatarajia kukamilika Februari 2024, Msimamizi wa Mradi una kazi ya ziada ya kufanya,” amesema Nombo

Nae Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam Prof. Preksedis Ndomba amesema Taasisi hiyo inatekeleza miradi mbalimbali ikiwemo Mradi wa Maendeleo wa kuanzisha Kituo cha Umahiri wa TEHAMA cha Kikanda cha Afrika Mashariki (RAFIKI) kupitia mradi wa EASTRIP ambapo kiasi cha Sh Bilioni 37 zinatumika kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu, uboreshaji maeneo mbalimbali ya utendaji, usimamizi wa Taasisi, uboreshaji wa mitaala, kuendeleza walimu na kuongeza udahili kwa wanafunzi wa kike kutoka ndani ya nchi na ukanda wa Afrika Mashariki.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Mshauri elekezi Mhandisi Musenyera Geophrey kutoka Kampuni ya Arqes Africa Ltd amemweleza Prof. Nombo kuwa hawana changamoto katika utekelezaji wa miradi hiyo na kwamba ujenzi wa Kituo cha Umahiri wa TEHAMA cha Kikanda cha Afrika Mashariki (RAFIKI) kimefikia asilimia 15 huku ujenzi wa mabweni ukifika asilimia 17 huku akisisitiza watahakikisha ujenzi huo unakamilika kulingana na muda uliopangwa.