*Ni kutokana na mabadiliko makubwa ya kiutendaji yaliyoongeza ufanisi ndani ya muda mfupi, wavutiwa uwekezaji kwenye miundombinu na vitendea
Na Mwandishi Wetu, TimesmajiraOnline
UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umetembelea maeneo ya uwekezaji katika Bandari ya Dar es Salaam uliofanywa na kampuni ya DP World na kusema uwekezaji huo umeleta mabadiliko makubwa ya kiutendaji na ufanisi mkubwa bandarini hapo kwa maendeleo na ustawi wa nchi.
Akizungumza mara baada ya ziara ya kutembelea Bandari ya Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Taifa wa UVCCM, Mohamed Kawaida aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wa kizalendo wa kuruhusu uwekezaji huo ambao una manufaa makubwa kwa taifa.
Alisema ripoti ya utendaji iliyowasilishwa na uongozi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imeonesha kuongezeka kwa ufanisi na kazi ya upakuaji na usafirishaji wa mizigo bandarini hapo tofauti na hofu iliyokuwepo hapo awali na watu waliokuwa wanapinga uwekezaji huo.
“Tukiwa kama wasimamizi wa Serikali katika utekelezaji wa ilani ya CCM, tumeamua kutembelea Bandari ya Dar es Salaam kujionea shughuli mbalimbali zinavyofanyika na kufurahishwa na ufanisi wake baada ya uwekezaji mkubwa kufanyika,” amesema Kawaida.
Alisema lengo kubwa la ziara hiyo ambayo pia ilihusisha Wenyeviti na Makatibu wa Umoja wa Vijana kutoka mikoa yote hapa nchini, lilikuwa kujionea na kujifunzabnamna kazi zinavyofanyika bandarini hapo.
“Mimi na viongozi wenzangu wote wa UVCCM tumefurahishwa na tija ya uwekezaji huu katika Bandari ya Dar es Salaam,” alisema na kuongeza; kuwa hapa awali kulikuwa na maneno mengi ya upotoshaji kuwa uwekezaji huu hauna tija kwa taifa na Watanzania wengi wangepoteza ajira na wafanyabiashara kukimbilia bandari nyingine za nchi jirani
Alisema Mwekezaji DP World amewekeza fedha nyingi sana katika miundombinu na vitendea kazi uliochangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa shehena za mizigo katika bandarini,”alisema na kuupongeza pia menejimenti ya TPA.
“Lakini katika ziara hii tumejionea hali tofauti kabisa, ambapo ufanisi na upakuaji mizigo umeongezeka baada ya uwekezaji mkubwa wa miundombinu na vitendea kazi kufanyika,”alisema kiongozi huyo akiwa ameongozana pia na Kamati ya Utekelezaji ya Chama hicho katika ziara hiyo.
“Hii inamaanisha kuwa mapato yanayotokana na uwekezaji huu yameongezeka na kuwa na tija katika maendeleo ya nchi yetu,”amesema Kawaida na kuiongeza kuwa Tanzania imebarikiwa neema ya kuwa na bandari hiyo inayohudumia nchi mbalimbali zikiwemo Rwanda, Burundi, Congo DRC, Msumbiji na Zambia.
Alisema uwekezaji kama huo ulihitajika ili kuendeleza kukuza soka la biashara katika Bandari.
“Dhana ya nchi yetu ni kuingiza kipato kwa maendeleo ya nchi kupitia maboresho ya sekta ya usafirishaji wa miundombinu mbalimbali ikiwemo ya reli ya SGR ambayo pia tumeitembelea na kuridhishwa na maendeleo yake,” amesema.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi ya Mkurugenzi wa TPA, Plasduce Mbosaa, Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Mrisho Selemani Mrisho, alisema kuwa viongozi wa umoja huo wamefurahishwa na ufanisi unaofanywa na mwekezaji DP World bandarini hapo kama ilivyotarajiwa na kujifunza mengi wakati wa ziara hiyo.
Alisema ili kuleta ufanisi na tija, mwekezaji DP World ameweka vitendea kazi mbalimbali bandarini hapo katika kuhudumia shehena za mizigo bandarini hapo na kufanya ufufuaji wa mashine (SSG) ambazo hapo awali zilikaa muda mrefu bila kufanya kazi kwa sababu ya matatizo ya umeme, lakini sasa hivi mwekezaji anazalisha umeme kupitia mashine hizo.
Lakini pia mwekezaji ameweka mashine za kuhudumia makasha katika uboreshaji wa miundombinu hiyo.
Alitoa wito kwa wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi kuendelea kuitumia bandari hiyo kutokana na mageuzi makubwa yanayofanyika katika kuharakisha kazi ya upakiaji na upakuaji wa mizigo bandarini hapo.
Ripoti ya utendaji kazi wa bandari hiyo iliyowasilishwa wakati wa ziara hiyo kwa viongozi wa umoja huo imeonyesha mafanikio makubwa yamepatikana baada ya Serikali chini ya Rais Samia kuridhia uwekezaji wa DP World bandarini hapo.
Ripoti hiyo imeonesha kuwa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita (2020/21/22/2023), mapato ya Bandari ya Dar es Salaam yamekuwa yakiongezeka kwa wastani wa asilimia 27.2 kwa mwaka, kutoka kiasi cha shilingi bilioni 801.7 hadi trilioni 1.3 kwa mwaka wa fedha 2022/2023 kulikotokana na kuongezeka kwa shehena zikiwemo kutoka nchi za jirani.
Lakini pia ripoti hiyo imeonyesha kuongezeka kwa idadi ya meli kwa wastani wa asilimia 7.5 kwa mwaka, ambapo mwaka 2021/2022 meli 1,569 zilitia nanga bandarini hapo na mwaka 2022/2023 zilikuwa meli 1,743.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba