January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

UWAMARAUDAR waiomba Serikali iwatambue

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

CHAMA Cha Mafundi Rangi na Ujenzi mkoa wa Dar es Salaam (UWAMARAUDAR), wameiomba Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi kukitambua chama hicho ili kiweze kupiga hatua katika kuliletea Taifa maendeleo.

Chama hicho kilisajiliwa rasmi Julai 4,2021 kwa mujibu wa sheria za nchi, Ofisi ya msajili wa vyama Dodoma, chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani.

Mpaka sasa bado chama hicho kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kukitambua ili kifanye kazi kwa kujiamini.

Lengo kuu la kusajili chama hicho, Serikali na Taifa kwa ujumla wakitambue, na uwepo wa ‘UWAMARAUDAR’ mafundi wakifahamu chama chao ambacho kitakuwa mwarobaini wa changamoto zinazowakabili

Akizungumza na majira Mwenyekiti wa Chama hicho, Juma Chakusaga amesema mafundi wamekuwa wakipata changamoto nyingi huku wakikosa sehemu ya utetezi wao.

Hata hivyo amesema, wamekuwa wakifanya kazi kubwa lakini maisha yao hayaendani na kazi wanazozifanya, lakini uwepo wa Chama hicho watapata suluhisho la kukabiliana na changamoto zao pindi wanapokuwa kazini.

“Tunaomba Wizara ya ujenzi isikilize vilio na changamoto zinazotukabili, tunafanya kazi nyingi lakini tunaishi maisha magumu, tunaomba Serikali itutambue ili tuepuke dhana ya kufanya kazi bila kuaminika,” amesema Chakusaga.

Naye Katibu Mwenezi wa ‘UWAMARAUDAR’, John Peter Muhali amesema uwepo wa chama hicho mafundi wengi watafanya kazi kwa kujiamini pindi serikali itakapokitambua chama chao.

Muhali amesema, dhamira yao kuwatetea mafundi kwani asilimia kubwa wamekuwa wakiishi maisha magumu licha ya kuwa na kazi ambayo inainua kipato chao pamoja na uchumi wa nchi kwa ujumla.

Mbali na hivyo, pia Muhali amesema miongoni mwa changamoto ambazo wamekuwa wakikumbana nazo ni mafundi wa kike katika suala zima la unyanyasaji wa kijinsia.

“Kumekuwa na tabia ya kuwanyanyasa mafundi wa kike na wahusika wa majengo wanayoyajenga jambo ambalo linazalilisha mafundi hao.

“Ninakemea tabia ya kikatili wanaofanyiwa dada zetu wanapokuwa kwenye majukumu yao, hali inayochangia kuwadidimiza na kushindwa kutimiza malengo yao, naamini chama hichi pia kitakuwa chachu la kutatua tatizo hili,” amesema Muhali.

Amesema, kwa sasa wapo kwenye mchakato wa kukitangaza chama hicho nchi nzima ili waweze kupata idadi kubwa zaidi ya wanachama.