Na Penina Malundo, Timesmajira
TABIA za Binadamu, Ongezeko la vyombo vya uvuvi na wavuvi wengi ziwa Victoria zimetajwa kuwa chanzo kimojawapo cha upungufu wa samaki katika ziwa hilo kwa miaka ya sasa.
Hali hiyo inasababisha uchumi wa wavuvi wengi kudorola kutokana na upatikanaji wa sam aki kuwa wa changamoto na bei yake Mitaani kuzidi kuwa juu.Mwenendo wa Takwimu za Uvunaji wa Samaki katika Ziwa Victoria nchini Tanzania zinaonyesha kushuka siku hadi siku kutokana na changamoto hizo pamoja na mabadiliko ya tabianchi yanayofanya mvua zinazonyesha kutokuwa za uhakika.
Mwenendo huo unaonyesha kuwa kadri miaka inavyoenda hali ya upatikanaji wa Samaki inazidi kushuka ambapo Mwaka 2018 uvunaji wa Samaki ulikuwa tani 235,175.90 zenye thamani ya shilingi trilioni 1.105 zilivunwa na wavuvi 109.397 waliokuwa wakitumia vyombo 31,773.
Huku kwa mwaka 2019 uvunaji wa samaki ulikuwa tani 270,968.03 zenye thamani ya shilingi trilioni 1.273 zilivunwa na wavuvi 109.397 waliokuwa wanatumia vyombo takribani 31,773.Mwaka 2020 hali ya uvunaji wa samaki ulikuwa tani 274,888.94 zenye thamani ya shilingi trilioni 1.374 zilivuwa na wavuvi takribani 109,397 waliokuwa wanatumia vyombo 31,773 huku mwaka 2021 hali ya uvunaji wa samaki ulikuwa tani 302,827.92 zenye thamani ya shilingi trilioni 1.726 zilivuwa na wavuvi takribani 102,779 waliokuwa wanatumia vyombo 31,074.Kwa Mwaka 2022 hali ya uvunaji wa Samaki hao ulishuka hadi kufikia tani 293,686.56 zenye thamani ya shilingi trilioni 1.967 zilivuwa na wavuvi takribani 102,779 waliokuwa wanatumia vyombo 31,074.
Asilimia kubwa ya wavuvi wanaofanya shughuli zao katika mialo mbalimbali pembezoni mwa ziwa hilo wameonekana ndio miongoni mwa watu ambao usababisha uchafuzi wa mazingira na kujihusisha kwa uvuvi haramu uliopindukia.
Shirika la Kimataifa la Uhifadhi (IUCN), linaonyesha asilimia 20 ya aina zote za viumbe hai katika Ziwa Viktoria walibainika kuwa kwenye hatari ya kuangamia kutokana na uvuvi uliopita kiasi, wingi wa vyombo vya kuvua pamoja na shughuli za kibinadamu kuwa chanzo.Upoteaji wa samaki unatishia maisha ya watu takribani milioni 42 ambao wanaoishi Tanzania, Kenya, Rwanda na Burundi ambapo asilimia kubwa kati yao wanategemea shughuli zitokanazo na uvuvi.WASIKIE WENYEWEKanyala Rushamba (55), mkazi wa Sengerema mkoani Mwanza anasema hali ilivyo sasa katika ziwa hilo inazidi kutisha siku hadi siku katika shughuli za uvuvi.
Anasema maisha ya zamani ya wavuvi yamebadilika kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na miaka ya nyuma ambapo sasa wanapokwenda ziwani huambulia samaki wachache tofauti na zamani.Rushamba anasema miaka ya nyuma ilikuwa tofauti na sasa kwani walikuwa wakifanya shughuli za uvuvi kuanzia jioni saa 12 hadi alfajiri, ambapo walikuwa wakitoka na samaki wengi akitoa mfano kuwa kati ya 100 hadi 200 kwa siku.”Kasi za shughuli za kibinadamu katika ziwa letu zimekuwa zikiongezeka mara kwa mara na shughuli hizo zinafanywa na wavuvi wenyewe wanaoenda kuvuta samaki,” anasema.
“Utakuta mvuvi anaingia ziwani tangu asubuhi mpaka jioni,bado hapo wavuvi wale wanapoingia usiku nao wanaingia usiku kucha hadi alfajiri utapata wapi samaki kwa namna hiyo wavuvi ni wengi, vyombo vya kuvulia sasa samaki navyo vimekuwa vingi hivyo kusababisha samaki tunaowatafuta kupata wachache kutokana na ziwa kutokuwa na hali ya utulivu muda wote samaki kuvuliwa.
“Anasema asilimia kubwa ya watu sasa hasa vijana wanaona katika uvuvi ndo sehemu ya kujipatia fedha nyingi hali inayowafanya nao kujikita katika uvuvi na kuwa na ongezeko la idadi kubwa ya wavuvi nchini.
“Zamani nikiwa na miaka 18 hivi tulikuwa wavuvi wachache sana na samaki walikuwa sio biashara kubwa tofauti na miaka ya sasa imekuwa ni ajira hata vijana nao wanakimbilia huku na wanaona wanapata fedha kwa urahisi tofauti na kulima bustani au shamba,” anasema.
Anasema mvuvi anapoingia baharini anakutana na zaidi ya vyombo 50 vya kuvulia samaki katika mwambao mmoja tofauti na miaka ya nyuma kabisa na hali hii ndio inayochangia samaki kukimbia kwani utakuta muda wote wavuvi wakiwa wanatafuta samaki .”Dhana za kuvulia miaka ya nyuma zilikuwa tofauti kabisa na sasa kwani zilikuwa ni za mita 3 kwenda chini lakini teknolojia na mambo yanavyoenda nyavu zinazotumika sasa ni zenye mita sita hadi 12 ambazo zinaenda chini kabisa na kuvua hata samaki wadogo na kuharibu mazalia yao,” anasema.
Akizungumzia suala la mabadiliko ya tabianchi, Rushamba anasema imechangia kwa kiasi kikubwa samaki kupotea kwani mvua zinazonyesha zimekuwa hazieleweki.
Anasema hiyo nayo imekuwa sababu ya samaki kukimbia kwani viumbe hivyo hai vinatabia ya kuzaliana katika maji muafaka.”Misimu ya mvua kwa sasa haieleweki, tunashukuru Mamlaka ya hali ya hewa TMA inavyokuwa mstari wa mbele katika kutuhabarisha mienendo ya mvua,hivyo inatufanya wavuvi kuitumia ipasavyo,” anasema.
“Tunakuwa tayari tunajua kuwa hali ya mvua ipo hivi na hivi na kujua kipindi kipi kizuri cha kuingia baharini mara mvua inaonyesha kwani tunajua ndipo Samaki wanakuwa wanzaliana wengi.”
Anasema upungufu wa samaki unatokea katika miambao yote inayozunguka ziwa Victoria iwe Kenya,Uganda,Rwanda au Bcurundi hali hii ni sawa kwa wote kutokana na uvuvi kuigiliana.
“Watu tunaofanya shughuli za uvuvi tumeongezeka sana na uvuvi haramu kuongezeka kwa kutumia nyavu au makokoro hali inayopelekea kuvua samaki hadi wachanga na mazalia yake,” anasema.
Mchuuzi wa samaki katika duka moja la kitoweo hicho lililopo Ubungo, Dar es Salaam, Khatibu Ally anasema samaki wamekuwa wakipanda bei tofauti na miaka ya miaka ya nyuma.Anasema kwa sasa kilo moja ya samaki sato inauzwa kuanzia sh.10000 hadi 12000 huku Sangara wakiuzwa kw sh. 8000 hadi 9000 na hizi bei zinapanda kutokana na hali ya upatikanaji wa samaki ziwani kuwa mgumu.
“Zamani tulikuwa tunauza sato kwa bei ya chini ilikuwa Shilingi 7,000 kwa kilo mtu ananunua hata kwa sangara nayo ilikuwa 6,000 watu walikuwa wananunua, ila sasa ni tofauti kabisa,” anasema.
Aliyekuwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega akijibu swali la Mbunge wa Muleba Kusini, Dk Oscar Kikoyo katika kikao cha Bunge Februari 6, mwaka huu, aliyetaka kujua kiwango gani vikosi kazi (task forces) vimepunguza tatizo la uvuvi haramu katika ziwa hilo kwa miaka mitatu iliyopita, anasema doria zilizofanyika katika maeneo ya ziwa hilo zimepunguza vitendo vya uvuvi haramu, biashara ya samaki wachanga na utoroshaji wa mazao ya uvuvi kwenda nje ya nchi kwa asilimia 80.Ulega ambaye kwa sasa ni waziri wa wizara hiyo, alisema katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2017/2018-2019/2020, kikosi kazi kilifanya doria na operesheni katika maeneo mbalimbali ya Ziwa Victoria.
Anasema utekelezaji wa doria uliwezesha kukamatwa kwa zana haramu zilizokuwa zikitumika katika shughuli za uvuvi ikiwemo nyavu za makila 28, 867, makokoro 532, timba 262, nyavu za dagaa 257 pamoja na injini 10 na magari matano.Ulega alisema Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia sekta ya uvuvi inaandaa mkakati wa Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi unaolenga kudhibiti uvuvi na biashara haramu ya mazao ya uvuvi.
Anataja mkakati huo kuwa na vipaumbele vya muda mrefu na mfupi kwani utekelezaji wa mkakati utashirikisha wizara na taasisi mbalimbali zikiwemo Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ofisi ya Rais TAMISEMI, vyombo vya ulinzi na usalama, jamii za wavuvi na wadau wengine wa sekta hiyo zikiwa taasisi zisizo za kiserikali (NGO na CBO).Pia alisema sekta ya uvuvi imeanzisha vituo vya doria 16) katika Ziwa Viktoria ikiwemo maeneo ya mipakani ili kuimarisha shughuli za ulinzi na usimamizi wa rasilimali za uvuvi na kudhibiti mianya ya utoroshaji wa mazao ya uvuvi kwenda nje ya nchi.”Vituo hivyo viko katika Mkoa wa Mwanza itatu, Mkoa wa Simiyu kimoja, Mara vitatu, Geita kimoja na Kagera vinane na kwa sasa Serikali inaendelea kutoa elimu kwa wavuvi ili kuondokana na matumizi ya zana haramu ambazo zinatishia kupungua kwa samaki katika maji ya asili,” anasema.
Katibu wa Kitengo cha Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi Mwambao wa Ziwa na Bahari (BMU), Maneno Hamis anasema shughuli za kila siku za binadamu zinachangia kwa asilimia 80 ya uharibifu wa mazingira.”Tunapambana na sheria sijui ni ndogo ndo maana wavuvi wamekuwa wakizipuuzia kwa mfano kutupa taka ziwani ambapo uchafua mazingira ya samaki na kuharibu mazalia yao,” anasema.
“Utakuta wavuvi wanavua Samaki kwa nyavu zenye asili za plastiki ambazo uwa haziozi na zikiisha kutumika utupa katika maji wanasahau samaki ni kiumbe kinachohitaji kukua katika mazingira safi endapo kinachafuliwa mazingira kinashindwa kuzaliana ipasavyo.”anasema.
Hamis anasema miongoni mwa nyavu ambazo zimekuwa zikiharibu mazingira ni pamoja na zile zinazofahamika kama timba na huingia nchini kutoka Uganda na huwa ni ngumu kuoza, na wavuvi wengi wanapenda kuzitumia kutokana na bei yake kuwa chini.
“Uvuvi haramu kutumia nyavu aina timba umekua kwa kasi sana Tika mialo ya ziwa Victoria ambapo nyavu hizi uwa haziozi hata zikikaa miaka 100 bali uja kugeuka kuwa sumu kwa samaki,” anasema”Nyavu za timba hunasa samaki wadogo na kusababisha kuharibu mazalia,” anasema.
Anasisitiza kuwa mojawapo wa majukumu yao kama BMU ni kulinda mazingira yote yasichafuliwe, kutunza vyanzo vya maji na mazalia ya samaki.”Hivyo tunajitahidi kadri ya uwezo licha ya kuwa na changamoto mbalimbali kama BMU na vifaa vya miundombinu ya ulinzi katika mialo tuliyopo,” anasema.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi,Prof. Riziki Shemdoe anasema Wizara ya Mifugo na Uvuvi utafiti kuhusu wingi wa samaki uliofanyika kupitia Taasisi za Kusimamia Uvuvi Ziwa Viktoria (LVFO), makisio ya kiasi cha samaki (fish stock) kilichopo katika maji ya ziwa hilo kinakadiriwa kuwa tani 2,678,512.Aidha, anasema katika kipindi cha mwaka 2022 tani 293,686.56 za samaki zenye thamani ya Shilingi trilioni 1.97 zilivunwa na wavuvi 102,779 waliokuwa wakitumia vyombo 31,074.
”Samaki waliovunwa katika ziwa hilo walichangia asilimia 62 ya samaki wote waliozalishwa nchini katika kipindi hicho, huku upande wa Tanzania likiwa na mialo 580,”anasema.
More Stories
TASHICO,yatoa ufafanuzi Mv.Serengeti kutitia upande mmoja
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua