Na. Mwandishi Wetu
Wananchi wa Wilaya ya Uvinza wamejengewa uwezo juu ya masuala ya menejimenti ya maafa nchini huku wakikumbushwa kujiandaa na kukabiliana na athari zinazoweza kutokea kutokana na mvua za El nino zilizotabiriwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini TMA zinazotarajiwa kunyesha kuanzia mwezi Oktoba hadi Desemba 2023.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Semina ya Kujenga Uelewa juu ya Upunguzaji wa Madhara ya Maafa katika Jamii Naibu Kamishna Hamisi Rutengo kutoka Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu amesema serikali imeendelea kutoa elimu juu ya kujikinga na madhara hayo kwa kuzingatia utabiri uliotolewa hususani kwa mikoa 14 inayotajwa kupata vipindi vya mvua juu ya wastani.
Semina hiyo ilihusisha Wajumbe kutoka katika ngazi ya Kijiji na Kata ambazo ni Uvinza, Kazulamimba na Kandaga upande wa vijini ni pamoja na Mwamila, Mazugwe, Kazuramimba, Nyanganga, Kalenge, Kandaga na Mlela iliyofanyika ukumbi wa Hospitali ya Wilaya ya Uvinza Mkoani Kigoma.
Naibu Kamishna aliongezea kuwa ni wakati sahihi kwa jamii kuendelea kuchukua tahadhari ikiwemo kuhama maeneo ya mabondeni, kuendelea kusafisha mitaro ya maji pamoja na kufuatilia taarifa zinazotolewa na mamlaka husiki ili kuendelea kuwa na jamii stahimilivu kwa maafa.
Aidha aliwakumbusha kuwa jukumu la maafa ni la kila mmoja katika nafasi yake kwa kuzingatia madhara yatokanayo na maafa.
“Kila mmoja anajukumu la kuendelea kukabilia, kujiandaa na maafa hivyo, katika maeneo yetu tuendelee kujilinda na kulinda wengine,” alisema Naibu Kamishna huyo.
Kwa Upande wake Mratibu wa Maafa Mkoa wa Kigoma Bw. Msafiri Nzunuri alieleza kuwa mkoa umekuwa ukikabiliwa na maafa mbalimbali ikiwemo Upepo mkali, mafuriko, mioto, pamoja na wanyama wakali ikiwemo Tembo na Viboko kwa maeneo tofauti tofauti na kushukuru elimu iliyotolewa na kusema kuwa itasaidia kuleta hamasa kwa jamii kuwa na utayari katika kukabiliana na maafa.
“Ofisi ya Waziri Mkuu imetupa heshima mkoa wetu kutoongezea maarifa ya namna ya kukabiliana na maafa, itumieni semina hii kwa manufaa na tija katika maeneo yenu, pia msizipuuze taarifa za utabiri wa hali ya hewa nchini,” alisema
Aliongezea kuwa Mkoa umeendelea kuweka mikakatu thabiti ya kuhakikisha inakuwa na uwezo wa kuyakabili maafa katika nafasi yake endapo yatatokea.
Naye mratibu wa Maafa Wilaya ya Uvinza Bw. Daniel Yowas akieleleza namna walivyojiandaa katika ngazi ya Wilaya alisema, Zipo kamati za maafa zenye uwezo mkubwa wa kushughulikia masuala hayo huku akizikumbusha kuzingatia elimu iliyotolewa na Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, na kuahidi kuendelea kuyafanyia kazi maelekezo na ushauri wa kitaalam unaotolewa kwa manufaa ya wananchi wote kwa ujumla na kutoa rai kwa kamati hizo kuendelea kutoa taarifa sahihi za tathmin ya majanga na kwa wakati.
Awali akitoa neno la utangulizi Mwakilishi kutoka Shirika la Kimataifa la Uhamaji (IOM) Bw. Reuben Mbugi ambalo limefadhili programu hizo ameeleza kwamba wataendelea kushirikiana na Serikali katika kuwafikia wananchi ili kuimarisha utayari wa kukabiliana na maafa nchini.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakaniÂ
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best